Makala

Askari rungu wataka watengewe saa za kunywa pombe mchana  

April 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa askari rungu Mlima Kenya (CRSGWA) maarufu kama ‘soja’ sasa unamtaka Naibu Rais Rigathi Gachagua awatengee saa mchana kunywa pombe kwa kuwa usiku wao huwa kazini.

Wameteta kwamba amri ya Bw Gachagua kwamba baa ziwe zikifunguliwa kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa tano usiku, imewabagua kwa kuwa huo ni wakati wao kuripoti kazini.

Wameteta kwamba ikiwa kwa uhakika serikali inadhamini msemo kwamba pombe ni baada ya kazi wala sio badala ya kazi, basi saa za kulewa za askari rungu zitengewe nafasi mchana wala sio usiku.

“Tungekuwa na uwezo tungetafuta wakili na tuishtaki serikali kwa kutubagua kwa msingi wa kazi yetu. Lakini kwa kuwa sisi ni wanyonge wasio na uwezo wa kujitetea kwa pesa au kupitia wanaharakati, tutamuomba tu Bw Gachagua kwa upole atuchungie mailahi na atutengee saa zetu za kuburudika,” Katibu wao Bw Harrisson Gachanja akaambia Taifa Dijitali.

Akizungumza Aprili 14, 2024 Mjini Karatina, Bw Gachanja alisema kwamba “saa ambazo Bw Gachagua anasisitiza ndizo faafu zaidi kwa watu kushiriki ulevi, ni hatari kwetu kama masoja”.

Alisema kwamba kwa kawaida mabawabu wengi wa usiku hutokea kazini saa moja asubuhi na kurejea saa nne jioni.

“Ina maana kwamba saa yetu ya kulewa baada ya kazi ni kuanzia saa moja ya asubuhi hadi saa nne asubuhi ili tulale muda wa saa sita, hadi saa nne jioni tuingie kazini tukiwa ulevi umetuondoka kichwani,” akasema.

Katika amri ya Bw Gachagua, askari rungu labda wawe wakijificha kazini na kuingia kwa baa ambapo watameza pombe yao harakaharaka na kisha warejee kazini kupambana sambamba na ulevi na kazi.

“Hali hiyo ni hatari kwa kuwa kazini tutakosa uwajibikaji na tukosane na wateja, pamoja na waajiri wetu. Aidha, tutaweka maisha yetu na ya tunaolinda hatarini kwa kuwa mlevi kazini hatakuwa na ule umakinifu wa kutambua wakora au kuchukua tahadhari ya kujiepusha na mabishano na majambazi wa kujihami,” akasema.

Katika hali hiyo, Bw Gachanja alishikilia kwamba sheria haifai kutungwa kwa msingi wa kutenga wengine akiongeza kwamba “tuko wengi ambao hufanya kazi usiku ni vile tu sisi ndio tunaoonekana zaidi”.

Alisema hakuna vile wengine watakuwa na uhuru wa kupiga sherehe kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa tano usiku, nao wengine wazimwe hadi ile siku watakuwa likizo.

“Ndio ina maana sisi kama askari rungu tunakemea hatua ya Bw Gachagua kutubagua pamoja na wengine wengi ambao hufanya kazi usiku. Kile angefanya ni kuzima utengenezaji na uuzaji wa pombe za mauti lakini ulevi atuachie sisi wenyewe tujidhibiti ndani ya baa bila vikwazo,” akasema.

Bw Gachanja alihofia kwamba masoja wengi wataanza kuvuta bangi ikiwa sheria ya Bw Gachagua haitakarabatiwa.

[email protected]