Habari Mseto

Askofu aanza msako wa kuwatimua mashoga na wasagaji kanisani

April 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WANYORO

MKUU wa Kanisa la African Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA) nchini, Askofu Julius Njoroge amewaamrisha Maaskofu na Makasisi kuanzisha operesheni ya kuwatimua kanisani mashoga na wasagaji kwa kukosa maadili.

Akizungumza wakati wa ibada ya kila mwaka ya upako katika kanisa la AIPCA Kiithe, Kaunti ya Meru, Askofu Njoroge alisema hawezi kuvumilia tabia hiyo ndani ya kanisa kwa kuwa ni kinyume cha mafundisho ya dini na tamaduni ya Afrika.

Askofu Njoroge alisema anaheshimu uamuzi wa juzi wa korti ulioruhusu makundi ya mashoga nchini kuunda miungano yao lakini akasisitiza mashoga hao hawakaribishwi katika kanisa hilo kwa sababu wataharibu maadili mema ya waumini wa AIPCA.

“Naamrisha hatua kali ichukuliwe dhidi ya muumini yeyote anayehubiri kuhusu ushoga au mwanachama wa kundi la mashoga. Tabia zao ni kinyume na maadili ya kanisa letu amalo linatoa mafunzo kuhusu maadili. Ushoga pia ni kinyume cha tamaduni zetu kama Waafrika,” akasema.

“Muumini yeyote anayehusika na ushoga eti kwa sababu mashoga na wasagaji walipewa idhini ya kuunda miungano yao na korti, anafaa kuchukuliwa hatua kali ya kuondolewa kanisani. Maaskofu wetu wanafaa kutekeleza hilo,” akaongeza.

Kiongozi huyo wa kidini alisisitiza kuwa kanisa lina jukumu la kuhakisha kondoo wake wana maadili na mafundisho yake yanafaa kulingana na bibilia.

Gavana wa Meru Kiraitu Murungi ambaye alikuwepo kwenye ibada hiyo naye aliomba kanisa kuingilia kati na kutoa mwongozo wa kidini kwa waumini hasa baada ya kuongezeka kwa mauaji na dhuluma za kijinsia.

“Kanisa lina jukumu kubwa katika jamii na kwa sasa kuna mambo ambayo jamii inakosa, ndiyo maana mauaji na dhuluma zimeongezeka. Vita vya maneno kwenye mitandao ya kijamii na ndoa nyingi kuvunjika ni ishara tosha kwamba vijana wetu wamekosa mwongozo wa kidini unaofaa kutolewa na kanisa,” akasema Bw Murungi.

Hata hivyo, Bw Murungi alilalamikia rekodi mbaya ya uhalifu miongoni mwa baadhi ya watu wanaoibuka na kutawazwa kuwa viongozi wa makanisa, wanaofaa kuhubiri neno la mungu.

“Tumewaona watu waliokuwa majambazi sugu waliotumikia vifungo vya kushiriki wizi wa kimabavu au uhalifu mwingine mbaya wakifungua makanisa na kujiita maaskofu,” akaongeza Bw Murungi.