Makala

Askofu ahimiza upendo miongoni mwa wanajamii

March 10th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

VISA vya dhuluma na vita vya kijinsia kwenye uhusiano wakati wa kuchumbiana na ndoa si vigeni nchini.

Baadhi wamejipata kupitia ukatili na wengine hata kuuawa baada ya kutofautiana.

Kwa kiasi kikuu, visa hivyo vinatajwa kukithiri miongoni mwa vijana na walio kabla umri wa makamu.

Kulingana na Askofu Solomon Seroney, visa vya aina hiyo vitaepukwa ikiwa wahusika watathamini upendo.

Aidha, ‘upendo’ ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali, kuanzia hali ya nafsi ya binadamu hadi kwa Mungu.

Neno upendo, linatokana na kitenzi ‘kupenda’, ambacho kinaashiria hisia za juu kwa mtu au mwenzako kwa njia ya kumjali.

Askofu Seroney amesema kila mmoja akithamini neno hilo, visa vya unyama vinavyoshuhudiwa vitakuwa historia.

“Mungu alipoumba mbingu na nchi, na wanaoishi humo, alipenda ulimwengu ili kila anayemwamini asipotee. Kwa hayo, tunahimizwa tupendane kupitia mfano wake,” mhubiri huyo akasema mnamo Jumatatu katika hafla ya mazishi ya Mama Rose Taplilei, Kaunti ya Uasin Gishu.

Ukatili na dhuluma nyingi zinachangiwa na mgogoro unaohusisha pesa na mali. Askofu Seroney alisema ni muhimu tufahamu kuwa pesa na urithi, tutayaacha hapa duniani, na Mwenyezi Mungu ametujaalia na ataendelea kutujaalia ili tumtumikie kwa hali na mali.

“Hakuna mali yatatupeleka mbinguni, Mungu ametujaalia nayo ili tumfanyie kazi,” akasema Mtumishi huyo wa Mungu. “Tenda mazuri ukiwa hapa duniani. Wanaume tupende bibi zetu, badala ya kuwapitishia mambo maovu tunayoshuhudia kila wakati, tuwaonyeshe mapenzi tuwaongezee upendo,” akasema.

Kwa mafumbo, Askofu Seroney alisema tofauti zinazoonekana kushuhudiwa kwenye mchakato mzima wa ripoti ya tume ya maridhiano, ndiyo BBI, zitasuluhishwa kwa njia ya maelewano na upendo kwa taifa.

Alisema upendo ukishamiri, taifa litaweza kuwaza kwa pamoja na kuweka sambamba mikakati itakayosaidia kuinua kila mwananchi.

Mama Rose Taplilei na ambaye aliaga dunia mwishoni mwa Februari akiwa na umri wa miaka 84 katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi, MTRH, baada ya kuugua Saratani kwa muda mrefu, alitajwa kama kielelezo katika jamii.

“Nyanya alituonyesha kupenda, hakubagua yeyote. Alisaidia kila mmoja katika familia na jamii na kijijini,” Samuel Kipchumba, mjukuu alimuomboleza.

Katika mahubiri yake, Askofu Seroney alisema kila mmoja akiiga nyayo za Mama Rose ambaye alimiminiwa sifa chungu nzima za upendo na ukarimu, visa vya dhuluma na ukatili kwenye uhusiano na ndoa vitafikia kikomo.