Askofu aonya wanaume dhidi ya kutumia ‘viagra’ kusisimua mapenzi

Askofu aonya wanaume dhidi ya kutumia ‘viagra’ kusisimua mapenzi

PIUS MAUNDU na LEONARD ONYANGO

MKUU wa Kanisa la Good News Church of Africa (GNCA) Raphael Kituva ameonya wanaume dhidi ya kutumia tembe za kuchochea mapenzi.

Kasisi huyo alisema kuwa wanaume wanafaa kuchukua tahadhari ili kuepuka maafa ambayo yamekuwa yakisababishwa na matumizi ya tembe hizo wakati wa kufanya mapenzi.

“Wanaume waotumia tembe wakati wa mapenzi wanajitakia kifo cha mapema. Komeni kutumia tembe kusisimua mwili,” akasema askofu huyo.

Alikuwa akizungumza kijijini Kibarani, Kaunti ya Makueni, wakati wa hafla ya mazishi ya Blantina Nduku Kamali aliyekufa katika ajali ya barabarani. Alikuwa muumini wa kanisa la GNCA.

Hivi karibuni kumekuwa na visa vingi vya wanaume, hasa wazee, kupatikana katika majumba ya wageni wamefariki baada ya kutumia tembe za kuongeza nguvu za kiume, almaarufu viagra.

Kisa cha hivi karibuni, kilitokea mjini Ntimaru, Kuria Mashariki, Migori ambapo mwanaume, 59, alipatikana amefariki katika chumba cha wageni baada ya kumeza tembe za kuongeza nguvu za kiume lakini mpenzi wake akakataa kushiriki mapenzi.

Kulingana na ripoti, mwanaume huyo alikuwa ameweka tembe hizo ndani ya soda aliyokunywa mara tu baada ya kuwasili kwenye lojing’i akiwa na mwanamke aliyeaminika kuwa ‘mpango wake wa kando’.

Mwanamke huyo alikataa kushiriki mapenzi na badala hivyo mzee huyo akalemewa na tembe hizo na hatimaye akaaga dunia.

Wataalamu wanasema kuwa tembe za Viagra zinaweza kusababisha kifo cha ghafla iwapo mtumiaji atakuwa anatumia dawa za kisukari, shinikizo la damu kati ya maradhi mengineyo.

You can share this post!

Makuhani wa usaliti

Mungu ni mkuu, asema mkurugenzi baada ya kuondolewa...