Habari Mseto

Askofu Kiengei: Msiokoke asilimia 100 kwa 100, bakisheni nafasi kukabiliana na wajinga

January 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

ASKOFU Ben Kiengei wa Kanisa la Jesus Compassion Ministry (JCM), Kiambu, Jumapili, Januari 7, 2023 alihimiza wakristu kujibakishia asilimia kidogo ya ukaidi kukabiliana na watu wenye nia kuwarejesha nyuma kimaendeleo.

Alisema, mtu hapaswi kuokoka asilimia 100 kwa 100 akipendekeza kujibakishia nafasi kidogo ya utoro kukabiliana na wajinga na wapuuzi maishani.

Askofu Kiengei ambaye ni mcheshi pia akihudumia kampuni ya Mediamax kupitia redio cha redio cha Kameme alisema kwamba “huu ni mwaka wa Mungu kutuondolea giza, kutuweka kwa mwangaza na kisha atupe form – mpango”.

Kwenye mahubiri yake huku akishangiliwa na waumini wake, alisema kwamba “hata katika taifa hili, huyo ameletwa kutuwekea giza tuondolewe”.

Krisimasi 2023 (Desemba 25) Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alichangia kanisa hilo Sh1 milioni za kufadhili mahitaji ya wanyonge chini ya utunzi wa washirika wa dhehebu hilo.

Askofu Kiengei akihuburi katika kanisa lake lililoko Ruiru, kwenye ibada ambayo ilihudhuriwa na kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Bw Maina Njenga na pia kiongozi wa wachache bunge la kitaifa Bw Opiyo Wandayi, alisema ombi lake mwaka huu, 2024, ni Mungu aondolee Kenya “giza ambalo linakwamisha maendeleo na kulemea wananchi”.

Ni ibada ambayo ilihudhuriwa pia na makachero wengi wakivalia kiraia kama ilivyothibitishwa na Kamanda wa polisi Ruiru, Bw Alexander Shikondi.

“Tuko na tumefika tena kwa wingi. Kando na kulishwa kiroho kazi yetu ya kudumisha amani na pia kujipa ufahamu wa matukio yatakayojiri lazima iendelee. Hawa wageni, waumini na mali yao wanahitaji usalama na sisi kama maafisa wa polisi ndio wamepewa wajibu wa kutoa huduma hiyo,” akasema.

Askofu Kiengei alisema kwamba atazidi kuwapokea wanasiasa kwa kuwa “wao sio ng’ombe na wanahitaji pia kulishwa kiroho”.

Alisema kuwa kando na kuwa na mtindo wa kupokea washirika wa upinzani, wengine wote wana uhuru kufika katika kanisa lake kushiriki ibada.

Hata hivyo, aliwatahadharisha waumini wake dhidi ya kuokoka asilimia 100 akisema “unafaa kubakisha nafasi kidogo ya utoro kukabiliana na wajinga na wapuuzi katika maisha”.

Akitambulisha bibi yake kwa Kalonzo, Askofu Kiengei alizua msisimko alipohoji aliamua kujitafutia ‘kasichana’ kadogo kazuri kwa sababu mtu akifanikiwa hapaswi kula nyasi ngumu kukiwa na ile nyororo malishoni.

 

[email protected]