Habari Mseto

Askofu mbakaji kusota jela miaka 75

December 19th, 2018 1 min read

Na RUSHDIE OUDIA

MAHAKAMA ya Kisumu jana ilimpa askofu kifungo cha miaka 75 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kunajisi watoto watatu na kumwambukiza mmoja wao Ukimwi kusudi.

Askofu Joseph Agutu Obala alipatikana na makosa kwa mashtaka manne, ambayo hakimu aliamua hukumu yake ni miaka 20 gerezani kwa kila kosa kati ya matatu ya kwanza ya unajisi, na miaka 15 kwa kumwambukiza mwathiriwa mmoja Ukimwi.

Huku akisoma uamuzi wake, Hakimu Mkazi, Bi Pauline Mbulika alisema hukumu hizo zitaandamana.

Bw Obala alipatikana na hatia ya kuwanajisi wasichana watatu ambao walikuwa wakiishi naye katika makao ya watoto mayatima Kisumu. Ilisemekana alimwambukiza mmoja wao Ukimwi kimakusudi wakati wa uhalifu huo uliotendekea kati ya Aprili na Julai 2016, na wakati mwingi alikuwa akiwapapasa isivyostahili.

Wasichana wawili walikuwa na umri wa miaka 15 na mmoja miaka 14.

Kulingana na stakabadhi zilizo mahakamani, mshtakiwa aliwapapasa wasichana hao isivyofaa katika siku tofauti kati ya Aprili na Julai 12, 2016.

Kiongozi huyo wa kanisa alijitetea kwamba mashtaka hayo yalikuwa ya uongo. Alidai watatu hao walikuwa na wapenzi wa kiume na walikuwa na tabia ya kutumia simu yake kuwasiliana nao kila mara alipokuwa hayuko karibu.

Aliongeza kuwa hapakuwa na ushahidi wowote kuthibitisha yeye ndiye aliyemwambukiza mmoja wao Ukimwi.

Wakili Steve Aoko ambaye anatarajiwa kufuatilia kesi ya mshtakiwa huyo alisema atakata rufaa kwa uamuzi wote uliotolewa.

Alisema wataangalia kama sheria ilifuatwa kikamilifu na kama kuna makosa yaliyotendwa wakati wa kesi.

“Askofu ni raia wa kawaida na huenda hakufahamu masuala mengine wakati wa kesi. Hayo ndiyo tutaangazia wakati tutakapokata rufaa,” akasema Bw Aoko.