Habari Mseto

Askofu na pasta kizimbani kwa madai ya ulaghai

November 7th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ASKOFU na Pasta wa Kanisa la Redeemed walishtakiwa Jumanne kwa kulaghai kanisa uwanja wa kanisa katika mtaa wa Kayole kaunti ya Nairobi.

Askofu William Nyamu Joseph, Pasta John Njeru Ndungo pamoja na washukiwa wengine watatu walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Martha Mutuku.

Walikanusha mashtaka matatu ya ulaghai wa shamba hilo la kanisa.

Askofu Joseph, Pasta Ndungo na Bw Andrew Gitonga M’Taramba, Bi Mellon Ng’endo Maina na Bi Florences Wanjiku Tiras walikanusha mashtaka matatu dhidi yao na kuomba waachiliwe kwa dhamana.

Washtakiwa hao watano walikana kuwa kati ya Januari 1 2012 na Oktoba 15 2012 walilaghai kanisa la Redeemed Church shamba lake nambari Plot No. D4-199.

Shamba hilo ni lile limejengwa kanisa la Redeemed mtaani Kayole kaunti ya Nairobi.

Shtaka la pili lilisema kuwa walijitengenezea cheti maalum cha kuwawezesha kuliuza shamba hilo wakidai kilitayarishwa na kampuni ya wakili Wandugi Karathe & Co,Advocates.

Shtaka la tatu lilisema kuwa watano hao walimkabidhi Naibu wa mkurugenzi wa masuala ya ardhi katika afisi ya kaunti ya Nairobi Bw Mwangi Chiera.

Afisi ya Bw Chiera iko katika mtaa wa Dandora Nairobi.

Cheti cha kuwaruhusu wauze shamba hilo walidai kilikuwa kimetayarishwa na wakili Wandugi Karathe.

Kesi itasikizwa Desemba 5 2018.