Habari Mseto

Askofu Njenga amiminiwa sifa tele katika misa ya kumuaga

November 6th, 2018 2 min read

Na WINNIE ATIENO

ALIYEKUWA Askofu mkuu wa kanisa la Katoliki John Njenga aliyeaga dunia Jumapili usiku atakumbukwa kama nguzo kuu ya kuunganisha viongozi wa kidini huko Pwani ili kupatanisha madhebebu tofauti.

Pia kiongozi huyo wa dini atakumbukwa kwa kupigia debe elimu hususan mtoto wa kike.

Hapo jana waumini wa Katoliki, makasisi na viongozi wa dini ya Kiislamu walimmiminia sifa marehemu wakisema kifo chake ni pigo kubwa.

Misa maalum iliandaliwa katika kanisa la Katoliki la Tudor ikiongozwa na kasisi Wilbard Lagho ambaye alimtaja marehemu kama nguzo kuu ya upatanisho wa madhehebu ya viongozi wa kidini huko Pwani.

“Marehemu Askofu Mkuu Njenga aliwahi kuwa mwenyekiti wa kongamano la maaskofu wa kanisa Katoliki nchini. Aliamini kuwa elimu ndio guzo kuu uwe maksini au tajiri elimu inawapatanisha nyote,” akasema kasisi Lagho.

Marehemu atakumbukwa kwa kujenga zaidi ya shule 50. Huko pwani alijenga shule ya wasichana ya upili ya St Teresa’s huko Chaani, shule ya upili ya Bishop Njega huko Taveta, kando na kupanua vituo vingine vya elimu.

“Aliamini kuwa elimu ndio inaweza kupatanisha watu ndio maana alijenga shule nyingi sana hususan kwa watoto wa kike. Alikuwa kiongozi ambaye aliamini katika uongozi, heri kutekeleza maamuzi aidha yawe mabaya au mazuri kuliko kuahirisha kuchukua hatua yoyote,” akasema.

Kasisi Lagho alisema atamkumbuka Askofu huyo kwa maneno, “Uamuzi mbaya ni bora kuliko kutochukua maamuzi yoyote.”

“Lakini cha msingi nakumbuka mapenzi yake ya elimu ambayo ilipelekea kufanikisha mimi kupata ufadhili wa elimu Ulaya kusomea Uislamu na lugha ya kiarabu, huko Roma,” akasema.

Alisema alikutana na askofu huyo mkuu Njenga mwaka wa 1989 miaka mitatu tu baada ya kusimikwa kama kasisi.

“Alikuwa anasisitiza kuwa heri kuishi na kufanya kazi na mtu aliyesoma kuliko yule aliyekosa elimu maanake inakuwa vigumu sana kukubaliana na swala lolote tata. Lakini ni rahisi kukubaliana na mtu mwenye elimu,” akasema Kasisi huyo.

Nalo Baraza la Maimamu na Wahubiri nchini (CIPK) likiongozwa na Katibu mwenezi wa baraza hilo, Sheikh Mohamed Khalifa alisema atamkumbuka marehemu kama mpatanishi mkuu.

“Alikuwa miongoni mwa viongozi waanzilishi wa upatanisho wa dini tofauti tofauti hapa Pwani. Aliunganisha na kupatanisha viongozi wa Kiislamu na wenzao Wakristo. Nitamkumbuka sana kwa hilo na ndio maana hata leo tuna muungano wa madhehebu ya viongozi wa kidini,” akasema Sheikh Khalifa.

Kasisi Lagho alisema marehemu aliamini kuwa walimu wanafaa wawe na tajriba ya dini kando na ile ya vyuo vya mafunzo ya elimu.

“Alinipata katika kanisa la Katoliki la Miritini akaniteua kusimamia seminari ya St Mary’s huko Kwale. Baadaye akanisaidia kupata elimu ya bure (scholarship) katika chuo kikuu cha Katoliki huko Nairobi,” akasema.

Alipomfuata na kumuelezea matumaini yake ya kusomea dini ya Kiislamu na lugha ya kiarabu, Kasisi Lagho alisema askofu huyo alimsaidia ndipo alipopata fursa hiyo huko Roma.

“Si mimi pekee ambaye alinisaidia, marehemu alisaidia makasisi wengi na viongozi wa kidini kupata elimu ya juu. Nakumbuka mwaka wa 2001, baada ya ghasia ya Kaya Bombo huko Likoni mwaka wa 1997 alianzisha baraza la pwani la viongozi wa kidini kutoka madhehebu mbali mbali kupatanisha waumini,” akasema Kasisi huyo.

Kwenye ghasia hizo za Kaya Bombo ambapo zaidi ya watu 200 waliuawa na mali ya mamilioni kuharibiwa, Kasisi Lagho alisema kisa hicho kiliwapatanisha viongozi wote wa kidini huko Pwani.

Viongozi hao wa kislamu na kikristo wakaenda kutoa msaada kwa waathiriwa wa ghasia hizo katika misikiti na kanisa.

Kwenye mahojiano Askofu huyo mkuu alisema ghasia hizo za Likoni zilikuwa changamoto kuu kuwahi kumfikia.

“Ni kutokana na hilo na uwamuzi wa kuunganisha viongozi wa kidini wakaamua kuanzisha baraza hilo ambalo ndilo la kipekee nchini,” alisema Kasisi Lagho addd.

Askofu mkuu wa Mombasa Martin Kivuva alithibitisha kifo cha Askofu Njenga aliyeaga dunia huko Nairobi jumapili usiku.