Habari Mseto

Askofu Pesa alia kupunjwa hela

October 14th, 2020 2 min read

CECIL ODONGO na RUSHDIE OUDIA

KIONGOZI wa Kanisa la Holy Ghost Coptic, John Pesa amelalamika kwamba alichezewa shere wakati wa kupokea pesa walizopewa walipozuru nyumbani kwa Naibu Rais William Ruto mnamo Jumatatu.

Askofu Pesa aliambia Taifa Leo jana kuwa licha ya hadhi yake, mahubiri mazuri aliyotoa nyumbani kwa Dkt Ruto eneo la Sugoi na mawaidha aliyompa, alipewa Sh10,000 pekee baada ya hafla hiyo.

“Nilipewa Sh10,000 ambapo Sh6,000 nilitumia kuweka mafuta kwenye magari mawili na nikasalia na Sh4,000. Hapo kwa pesa sikufurahia kwa sababu nimethibitisha kwamba maaskofu wengine walipewa pesa nyingi kuniliko. Hiyo ni tabia mbaya ambayo inafaa kukemewa kabisa kwa sababu matoleo hayo hayakufaa kutolewa kwa kubagua,” akasema Askofu Pesa.

Kiongozi huyo alikuwa kati ya viongozi wa kidini kutoka eneo la Nyanza waliomwombea Dkt Ruto nyumbani kwake Sugoi, mjini Eldoret mnamo Jumatatu.

Akizungumza na Taifa Leo jana kwa njia ya simu, Askofu Pesa alidai kupokea vitisho kutoka kwa watu asiowajua kwa kuzuru nyumbani kwa Dkt Ruto na kuhubiri.

“Tangu nitoke Sugoi sina amani. Nimekuwa nikipokea simu kutoka kwa watu wasiojulikana ambao wana msimamo wa kisiasa tofauti na ule wa Naibu Rais. Nimetusiwa na kutumiwa jumbe nyingi na sasa sijihisi salama tena kwa kuwa wanasema wanapanga kuniua,” akasema Askofu Pesa.

Alisema kwamba amekuwa akipigiwa simu na watu wasiojulikana wakimtusi na kutishia kuchoma kanisa lake jijini Kisumu.

VITISHO

“Wametishia kuja kunivamia hapa kwenye misheni yangu. Mimi naamini sikufanya kosa lolote kwa sababu anayetaka kuniua kutokana na masuala ya kisiasa anafaa kujua mimi ni kiongozi tu wa kidini. Jinsi tu nilivyoitwa kumwombea Naibu Rais, pia nitawaombea wengine nikiitwa,” akaongeza.

Hata hivyo, Askofu Pesa alieleza Taifa Leo kwamba hajutii kuwaongoza maaskofu wengine kumwombea Dkt Ruto, akisema hangekataa wito wa kiongozi wa hadhi serikalini kama Naibu Rais.

Alisema kuwa ameripoti vitisho hivyo kwa Idara ya Kuchunguzi Uhalifu (DCI), japo akasisitiza kuwa yupo tayari kwa lolote kwa kuwa hakutenda kosa kumwombea Naibu Rais.

Askofu John Pesa I (kati) alippongoza waumini katika maadhimisho ya kanisa lake mnamo Januari 13, 2020. Picha/Ondari Ogega

Pia aliomba msamaha kwa kunukuu visivyo kitabu cha Samueli 1:17 kwenye Bibilia, ambapo aliwashangaza wengi kwa kusema ni Mfalme Suleimani aliyemuua Goliathi. Kulingana na Biblia ni Mfalme Daudi aliyemuua Goliathi.

KUNUKUU BIBLIA VISIVYO

Mitandaoni, Wakenya walimkejeli na kumdhihaki Askofu Pesa kwa kunukuu bibilia vibaya, wakishuku iwapo aliteleza ulimi au hakufahamu alichokuwa akizungumzia.

Hata hivyo, alijitetea kuwa suala hilo halifai kutumiwa kumwonyesha kama mhubiri feki.

“Ulimi uliteleza na naomba msamaha kwa hilo. Mimi ni mtumishi wa Mungu ambaye amehubiri kwa miaka mingi na ninafahamu yaliyomo kwenye Bibilia,” akasema.

Aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha ubunge cha Kibra kwa tiketi ya ANC, Eliud Owalo ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, ndiye aliyewaongoza wahubiri kadhaa kutoka Nyanza kumtembelea na kumwombea Dkt Ruto.

Wengine walikuwa Askofu Calleb Olali (Kanisa la Nomiya), Askofu Johannes Angela wa Kanisa la Kianglikana la Bondo na Kasisi Julius Omoke wa Kanisa la Hera.

Wengine ni Kasisi George Gwada (Kanisa la New Pentecostal), Askofu Francis Obala (Kanisa la Fellowship Bible) na Kasisi Mkuu Reuben Odago (Kanisa la Baptist).