Michezo

Askofu Yohana: Tufunge kula na kunywa Arsenal ibebe taji la EPL

May 7th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

ASKOFU matata Yohana Gichuhi wa Kanisa la Christian Committed Gospel Church ambalo liko na matawi Nakuru, Murang’a na Kirinyaga, sasa amewataka mashabiki wa Arsenal wafunge kula na kunywa wakiombea timu hiyo itwae ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Amesema kinyang’anyiro kimefika katika mkondo wa lala salama.

“Ni Mungu tu atatekeleza mapenzi yake kwa kuwa kikombe cha EPL sasa Kiko mikononi mwake akituze apendavyo,”.

Askofu Yohana alisema kwamba Arsenal hata ishinde mechi zake mbili zilizosalia dhidi ya Manchester United na Everton, Manchester City nayo ishinde zake tatu dhidi ya Tottenham Hotspur, Fulham na West Ham United, taji litakuwa la Man City.

Kiwewe kikuu kwa Arsenal ni kibarua dhidi ya Man U, timu ambayo hutia bidii za mchwa katika pambano la kuwakutanisha.

Ndiposa Askofu Yohana akapendekeza mashabiki wa Arsenal wazingatie ni Mungu asaidie timu yao iibuke na ushindi nayo Man City iteleze.

“Ni lazima tuweke imani kwa Mungu kwa sababu hivi vita haviko mikononi mwetu sasa. TuMkumbushe Mungu wetu jinsi ambavyo tumejituma msimu huu wote kwa bidii na vile aMebariki Man City mara tano mfululizo,” akasema.

Aliwataka watu wa Arsenal wazingatie kuombea Tottenham Hotspur, Fulham na West Ham kwamba maombi yao ya kutaka kuibuka na ushindi dhidi ya Man City yajibiwe kwa kutendeka.

“Tutasaidia timu hizo kuomba ushindi na pia hata sisi tujikumbuke kwa kuhitaji ushindi katika mechi zetu. Kisha kwa unyenyekevu tuombe Mungu asambaze baraka za taji la EPL kwa timu nyingine kando na Man City. Hao wengine ni sisi wa Arsenal,” akasema.

Huku Arsenal ikiomba taji la EPL, hali halisi ni kwamba inaweza ikalipata, imalize ya pili au hata ya tatu nyuma ya Liverpool pia.

Ikiwa Man City itapoteza mechi zake, Liverpool ishinde zake mbili nayo Arsenal ipoteze zake mbili, basi Liverpool itaibuka bingwa.

Katika hali hiyo, wazo la Askofu la kuweka imani ya kujinyima chakula na maji ndio ushindi huo uwafikie linaonekana kuwa la busara na ambalo huenda likakumbatiwa na mashabiki wenzake.