Makala

Aspirin inaweza kupunguza maambukizi ya HIV – Utafiti

November 28th, 2018 2 min read

ELIZABETH MERAB Na PETER MBURU

IJAPOKUWA dawa ya Aspirin hutumiwa kupunguza uchungu wa mwili pale unapouma, sasa imebainika kuwa inaweza kutumika kupunguza maambukizi ya virusi vya HIV.

Watafiti walikagua dawa ya Aspirin na nyingine zinazotumiwa kupunguza maumivu kuona namna zinaadhiri shembechembe za mwili ambazo huvamiwa na virusi vya HIV na kupata kuwa wanawake waliozitumia walikuwa na uwezekano mdogo kuambukizwa virusi hivyo.

“Wakati seli za mwili zinaumwa huwa rahisi kuambukizwa virusi vya HIV lakini pale zinapotulia inakuwa vigumu. Kuwashwa huleta seli zinazopokea virusi hivyo karibu na sehemu ya uzazi ya mwanamke,” utafiti huo ukasema.

Utafiti huo ulihusisha wanawake 37 kutoka Kenya na wote walipimwa kabla na baada ya kutumia Aspirin, kwa kipindi cha hadi wiki sita.

Washiriki walipewa kiwango cha chini ama cha kawaida cha dawa hiyo kama tu jinsi hutumiwa kuzuia magonjwa mengine.

Kati ya dawa za kupunguza maumivu zilizopimwa, ni Aspirin iliyokuwa na nguvu zaidi ya kupunguza uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa huo. Aspirin ilipunguza kiwango cha seli zinazoambukizwa HIV katika sehemu ya uzazi ya mwanamke kwa asilimia 35.

Utafiti huo ulisema kuwa wengi wa wanawake ambao wamekaa miaka bila kupata ugonjwa wa HIV imekuwa kwa sababu ya sehemu zao za uzazi kukosa seli zinazowasha (ama maumivu) ambazo kwa kawaida ndizo huambukizwa maradhi hayo kwa kiwango kikubwa.

Dawa ya Aspirin ilionekana kuimarisha afya ya ngozi katika sehemu za siri za wanawake vilevile, jambo ambalo aidha linasaidia kupunguza maambukizi, kwa kuzuia virusi vya HIV kupenyeza kwenye damu.

“Utafiti zaidi unaahitajika kudhibitisha matokeo yetu na kupima ikiwa kiwango hiki kinaweza kupunguzwa katika maisha ya kila siku,” akasema mtafiti mkuu Dkt Keith Fowke.

Mtafiti huyo alisema kuwa hiyo inaweza kuwa njia bora zaidi ya isiyo ya gharama kubwa kwa watu kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo hatari.

Aidha, ikifanikiwa kutibu Aspirin itakuwa dawa ya kwanza inayolenga kuimarisha ubora wa kinga kwa mlengwa wa virusi, badala ya kulenga virusi vyenyewe kama visa vya mbeleni.