Michezo

Aston Villa kumsajili kipa Martinez kutoka Arsenal kwa Sh2.8 bilioni

September 13th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIPA raia wa Argentina, Emiliano Martinez, anatarajiwa kuagana na Arsenal na kurasimisha uhamisho wake hadi Aston Villa kwa kiasi cha Sh2.8 bilioni.

Martinez, 28, alikuwa tegemeo kubwa la Arsenal katika fainali ya Kombe la FA iliyoshuhudia kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kikiwapepeta Chelsea 2-1 uwanjani Wembley, Uingereza.

Kiini cha kubanduka kwa Martinez uwanjani Emirates ni maamuzi ya Arteta na benchi ya kiufundi ya Arsenal kusisitiza kwamba Bernd Leno ataendelea kuwa kipa wao chaguo la kwanza kwa mara nyingine muhula huu.

Martinez, ambaye tayari ametua uwanjani Villa Park kufanyiwa vipimo vya afya, atakuwa sogora wa tatu kuingia kambini mwa kikosi hicho muhula huu baada ya fowadi Ollie Watkins aliyetokea Brentford na beki Matty Cash aliyesajiliwa kutoka Nottingham Forest.

Martinez aliachwa nje ya kikosi cha Arsenal kilichotegemewa na Arteta dhidi ya Fulham katika mchuano wa ufunguzi wa EPL uliowashuhudia wakisajili ushindi wa 3-0 uwanjani Craven Cottage mnamo Septemba 12, 2020.