Aston Villa wadidimiza matumaini ya Spurs kuwa miongoni mwa washiriki wa soka ya bara Ulaya msimu ujao

Aston Villa wadidimiza matumaini ya Spurs kuwa miongoni mwa washiriki wa soka ya bara Ulaya msimu ujao

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Tottenham Hotspur kufuzu kwa soka ya bara Ulaya msimu ujao yalididimizwa na Aston Villa mnamo Jumatano baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 mbele ya mashabiki 10,000 katika uwanja wa nyumbani.

Huku tetesi kuhusu uwezekano wa fowadi na nahodha Harry Kane kuondoka kambini mwa Spurs zikishika kasi, mashabiki wa kikosi hicho walisikika wakiimba “Kane ni mmoja wetu” pindi baada ya kiungo Steven Bergwijn kumzidi maarifa beki Marvellous Nakamba na kuwaweka waajiri wake Spurs kifua mbele katika dakika ya nane.

Hata hivyo, wimbo huo wa kutaka Kane asitishe mpango wake wa kugura Spurs ulikoma ghafla katika dakika ya 20 baada ya Villa kusawazisha kupitia goli la beki Sergio Reguilon aliyejifunga baada ya kuzidiwa presha na Nakamba aliyemsughulisha pia kipa Hugo Lloris.

Ollie Watkins alizamisha kabisa chombo cha Spurs katika dakika ya 39 baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya Reguilon na Eric Dier.

Mbali na Bergwijn, wanasoka wengine wa Spurs waliomtatiza pakubwa kipa Emiliano Martinez wa Villa bila ya kufaulu kufunga bao ni Kane, Son Heung-min na Gareth Bale.

Wanasoka wa Spurs waliondoka uwanjani wakiwa wameinamisha vichwa kwa aibu huku wakizomewa na mashabiki wao. Kichapo hicho kiliwateremsha hadi nafasi ya saba baada ya West Ham kuwapiga West Brom 3-1.

Chini ya kocha mshikilizi Ryan Mason, Spurs kwa sasa wanajivunia alama 59 sawa na Everton ambao huenda wakaruka iwapo Spurs watazidiwa ujanja na Leicester City katika mechi ya mwisho msimu huu mnamo Mei 23 ugani King Power.

Villa wanaonolewa na kocha Dean Smith kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 jedwalini kwa pointi 52. Kikosi hicho kitamenyana na Chelsea katika mchuano wa mwisho ligini muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wachomea Rais picha

Juventus wapepeta Atalanta na kutwaa ubingwa wa Coppa Italia