Aston Villa wamtimua kocha Dean Smith kwa sababu ya matokeo duni

Aston Villa wamtimua kocha Dean Smith kwa sababu ya matokeo duni

Na MASHIRIKA

ASTON Villa wametimua kocha Dean Smith baada ya kudhibiti mikoba yao kwa kipindi cha miaka mitatu.

Smith, 50, anaondoka Villa baada ya Southampton kuwatandika 1-0 katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 5, 2021.

Hiyo ilikuwa mechi ya tano mfululizo kwa Villa kupoteza kwenye EPL msimu huu.

Kwa sasa wanashikilia nafasi ya 17 kwenye msimamo wa jedwali na wako katika hatari ya kuingia katika orodha inayojumuisha vikosi vitatu vya mwisho ligini.

Kwa mujibu wa Villa, mchakato wa kutafuta kocha atakayerithi mikoba ya Smith umeanza ila hawatakuwa na pupa ya kumwajiri mkufunzi wa kujaza pengo hilo.

Hata hivyo, kocha wa timu ya taifa ya Denmark, Kasper Hjulmand anahusishwa pakubwa na mikoba ya Villa ambao sasa wako chini ya uelekezi wa mkurugenzi wa soka, Johan Lange.

Hjulmand, 49, aliongoza Denmark kutinga nusu-fainali za Euro 2020 ambapo walichabangwa na Uingereza ugani Wembley.

Smith anakuwa kocha wa tano wa EPL baada ya Nuno Espirito Santo (Tottenham Hotspur), Daniel Farke (Norwich City), Xisco Munoz (Watford) na Steve Bruce (Newcastle United) kupoteza kazi katika kampeni za kivumbi hicho muhula huu.

Aliajiriwa mnamo Oktoba 2018 na akaongoza Villa kupandishwa ngazi kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) hadi EPL.

Licha ya Villa kusuasua katika msimu wa kwanza wa EPL chini ya Smith, kocha huyo aliongoza waajiri wake kutinga fainali ya Carabao Cup mnamo 2019-20.

Mnamo 2020-21, Villa waliambulia nafasi ya 11 kwenye EPL na ngome yao ikasalia kuvuja baada ya Manchester City kumtwaa kiungo Jack Grealish.

Tangu washinde Man-United mnamo Septemba 25, 2021 Villa hawajashinda mechi yoyote huku wakijizolea alama 10 pekee kutokana na mechi 11 za ufunguzi wa msimu huu.

Hiyo ndiyo rekodi mbovu zaidi kwa Villa kuwahi kushuhudia katika historia yao tangu Januari na Februari 2017 walipokuwa wakinogesha kipute cha Championship.

Smith anaagana na Villa baada ya kuongoza kikosi hicho kushinda mechi 28 kati ya 87 za EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wachungaji wapendekeza adhabu ya kiboko irejeshwe shuleni

Arsenal wakomoa Watford na kuingia tano-bora EPL

T L