Aston Villa wapepeta Leeds United na kuweka hai matumaini ya kushiriki soka ya bara Ulaya muhula ujao wa 2021-22

Aston Villa wapepeta Leeds United na kuweka hai matumaini ya kushiriki soka ya bara Ulaya muhula ujao wa 2021-22

Na MASHIRIKA

ASTON Villa walipepeta Leeds United 1-0 mnamo Jumamosi uwanjani Elland Road na kuweka hai matumaini ya kusakata soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Matokeo hayo yaliwapaisha Villa hadi nafasi ya nane jedwalini kwa alama 39, sita nyuma ya nambari nne West Ham United waliopokezwa kichapo cha 2-1 na viongozi Manchester City wanaopigiwa upatu wa kutwaa ufalme wa msimu huu.

Bao la pekee katika mechi iliyowakutanisha Villa na Leeds ya kocha Marcelo Bielsa lilifumwa wavuni na Anwar El Ghazi aliyeshirikiana vilivyo na Ollie Watkins katika dakika ya tano kabla ya kumwacha hoi kipa Islan Meslier.

Villa wanaonolewa na kocha Dean Smith walitamba katika mchuano huo wa ugenini licha ya kukosa huduma za kiungo na nahodha Jack Grealish anayeuguza jeraha la mguu.

Leeds United kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwa alama 35 baada ya kutandaza jumla ya michuano 26. Ni pengo la pointi nne ndilo linawatenganisha na Villa ambao kwa sasa wana kibarua kizito dhidi ya Sheffield United, Wolves na Newcastle United kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Niliwahi kujaribu kumsajili Bruno Fernandes wa Manchester...

Pigo kwa Barcelona fowadi Lautaro Martinez wa Inter Milan...