Aston Villa wapiga Man-United breki kali ligini

Aston Villa wapiga Man-United breki kali ligini

Na MASHIRIKA

MABINGWA mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester United walipigwa breki kali hapo jana na Aston Villa waliowacharaza 1-0 uwanjani Old Trafford.

Kiungo mvamizi raia wa Ureno, Bruno Fernandes alipoteza fursa maridhawa ya kusawazishia Man-United mwishoni mwa kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya kupaisha mkwaju wa penalti.

Tukio hilo liliwezesha Villa kushinda Man-United kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 12 katika uwanja wao wa nyumbani.

Bao la pekee na la ushindi kwa Villa lilipachikwa wavuni na Kortney Hause katika dakika ya 88. Masogora wa kocha Ole Gunnar Solskjaer walipokezwa kichapo hicho siku tatu baada ya West Ham United kuwabandua kwenye kivumbi cha Carabao Cup kwa kichapo kingine cha 1-0 ugani Old Trafford.

Man-United wameratibiwa sasa kuvaana na Villarreal mnamo Jumatano ijayo katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kukwaruzana na Everton na Leicester ligini kwa usanjari huo.

Sawa na Chelsea na Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa UEFA, Man-United kwa sasa wanajivunia pointi 13 kutokana na mechi sita za hadi kufikia sasa kwenye kampeni za EPL muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Bobi Wine azimwa kuelekea Amerika kwa kutotimiza masharti...

Wanafunzi kadhaa Juja washindwa kujiunga na Kidato cha...