Michezo

Aston Villa yaaibisha Liverpool katika EPL kwa kichapo kinono cha 7-2

October 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp amesema wanasoka wake wa Liverpool “walijiwekea historia mbaya” kwa kutepetea pakubwa na kuruhusu Aston Villa kuwadhalilisha kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani Villa Park mnamo Oktoba 4, 2020.

Liverpool walicharazwa 7-2 na kuweka historia ya kuwa mabingwa watetezi wa kwanza wa EPL kuwahi kufungwa mabao saba tangu Sunderland waipepete Arsenal 7-1 mnamo Septemba 1953.

Ollie Watkins alipachika wavuni magoli matatu naye Jack Grealish akahusika katika mabao matano kwenye gozi hilo lililoshuhudia Liverpool wakipoteza mchuano wao wa nne ligini tangu Januari 2019.

“Tulipoteza dira baada ya Villa kufunga bao la kwanza. Ni nani amewahi kutaka kupoteza mechi kwa kiasi hicho cha mabao?” akatanguliza Klopp.

“Miaka michache iliyopita, tulijiwekea malengo ya kuandikisha historia katika EPL, lakini historia hiyo haikuwa iwe aibu ya kudhalilishwa kwa kichapo cha 7-2.”

“Tulikuwa na nafasi nyingi za kurejea mchezoni baada ya bao la kwanza, ila kibarua kikawa kigumu zaidi mechi ilipoendelea. Sikuona hata uwezekano wa mechi hiyo kukamilika kwa sare ya 7-7.”

“Tulifanya makosa mengi makubwa na kupoteza mipira katika maeneo hatari. Safu ya nyuma ilishindwa kudhibiti makali ya wapinzani na tukasalia hoi kila mahali,” akasema Klopp kwa kusisitiza kwamba hakuna anayestahili kulaumiwa kwa matokeo hayo ila yeye mwenyewe na kikosi alichokipanga uwanjani.

Liverpool walijitwalia taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 mwishoni mwa msimu uliopita kwa kudumisha pengo la alama 18 kati yao na nambari mbili Manchester City.

Kinyume na msimu huu, Liverpool walipoteza mchuano wao wa kwanza wa EPL dhidi ya Watford katika mkondo wa pili mnamo Februari 2020.

“Tumeanza vibaya na sasa kila mpinzani atakuwa akijituma zaidi kuangusha Liverpool. Hata hivyo, muhimu zaidi ni jinsi tutakavyojinyanyua na iwapo tutafaulu kuweka kando maruerue na aibu ambayo Villa walitutia,” akaongeza Klopp ambaye ni raia wa Ujerumani.

Fowadi Mohamed Salah alifunga mabao mawili ya Liverpool na kufanya mambo kuwa 2-1 kisha 5-2 ila juhudi zake hazikutikisa Villa ambao chini ya kocha Dean Smith, walitawaliwa na ari ya kuwateremkia wageni wao vilivyo.

Mbali na kipa chaguo la kwanza Alisson Becker anayeuguza jeraha la bega, wachezaji wengine waliokosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Liverpool katika mechi hiyo dhidi ya Villa ni fowadi Sadio Mane na kiungo Thiago Alcantara wanaougua Covid-19.

Kwa mujibu wa Klopp, huenda Alisson akasalia nje kwa zaidi ya majuma manne baada ya kurejelewa kwa kivumbi cha EPL kitakachopisha mechi za kimataifa mwishoni mwa wiki hii.

Ina maana kwamba Liverpool wataendelea kutegemea huduma za kipa Adrian San Miguel aliyejiunga nao msimu uliopita kutoka West Ham United.

Baada ya kupepetana na viongozi wa jedwali Everton wikendi hii, Liverpool watawaendea Ajax katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kurejelea kampeni za EPL dhidi ya Sheffield United mnamo Oktoba 24, 2020.