Aston Villa yapiga Everton breki kali kwenye EPL

Aston Villa yapiga Everton breki kali kwenye EPL

Na MASHIRIKA

ASTON Villa walifunga mabao matatu chini ya dakika tisa za kipindi cha pili ugani Villa Park na kukomesha rekodi ya kutoshindwa kwa Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Wakiwa kati ya klabu tano pekee zilizokuwa hazijapoteza mchuano wowote kufikia Jumamosi ya Septemba 18, Everton walijikuta wakiwa hoi na kuzidiwa ujanja katika kila idara na hivyo kuwawezesha wenyeji kutia kapuni alama zote tatu muhimu.

Baada ya kipindi cha kwanza kukamilika bila bao lolote, mchuano huo ulipata msisimko zaidi katika dakika ya 66 baada ya beki Matty Cash kumzidi maarifa kocha Asmir Begovic katika dakika ya 66.

Everton walifungwa bao la pili dakika tatu baadaye kupitia kwa Leon Bailey aliyetokea benchi katika kipindi cha pili kushuhudia krosi yake ikijazwa na Lucas Digne katika wavu wao wenyewe.

Bailey alipachika wavuni bao la tatu la Villa kwa ustadi mkubwa katika dakika ya 75. Baada ya mwanzo mbaya katika kampeni za msimu huu, Villa wanaonolewa na kocha Dean Smith walisajili ushindi wa pili msimu huu na kupaa hadi nafasi ya 10.

Pigo la pekee kwa Villa katika mchuano huo ni jeraha baya ambalo sasa litamweka nje kiungo John McGinn.Nyota huyo raia wa Scotland aliondolewa uwanjani dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

McGinn aliendelea na mchezo baada ya kugongana na Michael Keane wakiwania mpira wa kona mwanzoni mwa kipindi cha kwanza. Hata hivyo, alionekana tena kulemewa baada ya dakika 20 kabla ya kuondolewa uwanjani ili kutathminiwa na madaktari.

Licha ya kuwatamalaki Burnley katika mchuano mwingine wa EPL mnamo Septemba 13, Everton walishindwa kutamba dhidi ya wenyeji wao ugani Villa Park huku wakielekeza kombora moja pekee langoni mwa Villa.

Kocha Rafael Benitez alilazimika kukifanyia kikosi chake mabadiliko matatu baada ya kipa Jordan Pickford na fowadi Richarlison Andrade kupata majeraha ya bega na goti mtawalia wakati wa mchauno wa awali dhidi ya Burnley.

Maandalizi yao dhidi ya Villa yalitatizwa zaidi baada ya nahodha Seamus Coleman kuachwa nje ya kikosi kutokana na jeraha la paja alilolipata wakati wa mazoezi mnamo Ijumaa.

Nafasi za watatu hao waliokuwa wamewajibikia Everton katika kila mchuano kabla ya kuvaana na Villa zilijazwa na Begovic, Alex Iwobi na Salomon Rondon aliyewajibishwa na Everton kwa mara ya kwanza baada ya kusajiliwa mwanzoni mwa muhula huu.

Villa kwa sasa hawajashindwa katika mechi tano za EPL dhidi ya Everton tangu warejee kunogesha kivumbi hicho cha haiba kubwa mnamo 2019. Kwa sasa wanajivunia rekodi ndefu zaidi ya kutoshindwa ligini ugani Villa Park tangu Januari 2015.

  • Tags

You can share this post!

Aston Villa yapiga Everton breki kali kwenye EPL

Man-City wapoteza pointi mbili muhimu za EPL dhidi ya...