Michezo

Aston Viulla wamasajili Ross Barkley wa Chelsea kwa mkopo

October 1st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ASTON Villa wamemsajili kiungo Ross Barkley kutoka Chelsea kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Barkley, 26, anajivunia kuvalia jezi za timu ya taifa ya Uingereza mara 33 hadi kufikia sasa. Nyota huyo amekuwa mchezaji wa Chelsea ugani Stamford Bridge tangu Januari 2018 alipoagana na Everton.

Sogora huyo amewajibishwa na Chelsea mara tatu pekee msimu huu na akafunga bao moja.

“Kupata huduma za mwanasoka wa haiba kubwa kama vila Barkley si jambo dogo. Naamini kwamba atajikuza vyema zaidi kitaaluma akiwa hapa na atatusaidia kuimarisha kikosi chetu,” akasema kocha wa Villa, Dean Smith.

Barkley aliondoka kambini mwa Everton mnamo 2018 baada ya kuchezea kikosi hicho cha Mersyside jumla ya mechi 179 tangu utotoni na kukifungia jumla ya mabao 27.

Kusajiliwa kwa wanasoka Kai Havertz, Timo Werner na Hakim Ziyech kulimweka Barkley katika ulazima wa kubanduka Stamford Bridge.

Barkley ambaye hajachezeshwa na Chelsea katika mchuano wowote wa EPL msimu huu, alifunga bao katika ushindi mnono wa 6-0 uliosajiliwa na kikosi hicho dhidi ya Barnsley katika Carabao Cup mnamo Septemba 23, 2020.

Barkley anakuwa mchezaji wa haiba kubwa zaidi kuingia katika sajili rasmi ya Villa muhula huu baada ya kikosi hicho cha kocha Smith kujinasia huduma za winga Bertrand Traore kutoka Olympique Lyon, mfumaji Ollie Watkins kutoka Brentford, kipa Emiliano Martinez kutoka Arsenal na beki wa kulia Matty Cash kutoka Nottingham Forest.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO