Habari Mseto

Asukumwa jela kwa kuiba kuku

July 9th, 2020 1 min read

Na Titus Ominde

MWANAMUME amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka miwili na mahakama mjini Eldoret baada ya kukiri shtaka la kuiba kuku watatu.Eliud Chege Njuguna, 29, alishtakiwa kwa kutenda kosa hilo mnamo Juni 27, katika kijiji cha Yamumbi, Kaunti Ndogo ya Kapseret, Kaunti ya Uasin Gishu.

Hakimu Mkuu Mwandamizi, Richard Odenyo alimhukumu mshtakiwa huyo baada ya kukiri kuiba kuku hao wa jirani.Akijitetea, aliambia mahakama alijutia kitendo alichokifanya huku akisema alikuwa mlevi wakati wa tukio hilo.

‘Naomba mahakama inisamehe kwa kile nilichofanya. Nilikuwa mlevi sikujua nilichokuwa ninafanya,’ alisema.Baada ya kusikiza malilio yake, mahakama iliendelea na kumhukumu mshtakiwa kwa miaka miwili jela.

‘Nimesikia malilio yako. Ninakuhukumu baada ya kukiri kosa lako mwenyewe. Utafungwa jela miaka miwili,” aliamuru hakimu.