Asukumwa jela miaka 5 kwa kumrusha mwanadada kutoka orofa ya 12 hadi ya tisa

Asukumwa jela miaka 5 kwa kumrusha mwanadada kutoka orofa ya 12 hadi ya tisa

NA RICHARD MUNGUTI

MAMBO yamemwendea mrama mtaalam wa masuala ya teknolojia (ICT) aliyemsababishia majeraha ya kudumu msichana aliyemchumbia katika mtandao wa Facebook.

Mtaalamu huyo mnamo Alhamisi alisukumwa jela miaka mitano bila faini.

Moses Gatama Njoroge aliyemfurusha Eunice Wangari Wakibi kutoka orofa ya 12 hadi orofa ya tisa baada ya mrembo kukataa kufanya tendo la ndoa alipelekwa moja kwa moja hadi gereza la Viwandani kuanza kutumikia kifungo.

Gatama aliyedai alikerwa na hatua ya Wangari kukataa wito wake hata baada ya kumnunulia maankuli ya mchana na Soda, aliomba korti imsamehe akisema “nilipandwa na mori baada ya ndoto yangu ya kula tunda kuambulia patupu.”

Kisa hicho cha Septemba 13, 2020 kiliwaudhi na kuwashtua wengi na hata jana Alhamisi hakimu alilaumiwa na mawakili kwa kutoa adhabu isiyo kali wakisema mshtakiwa alimpa majeraha ya kudumu Wangari.

Akimhukumu Gatama, hakimu alimweleza hatia aliyofanya adhabu yake ni kifungo cha maisha lakini kwa vile ameyaungama makosa yake na kuahidi kudhibiti hasira yake atamfunga miaka mitano tu.

Mahakama ilishutumu kitendo hicho cha mshtakiwa na kumtaka ajirekebishe akiwa jela.

Wakili Crispus Kabene aliyemtetea mshtakiwa aliomba mahakama itilie maanani umri mdogo wa mshtakiwa ambao ni miaka 34 ikipitisha adhabu.

“Mshtakiwa alimtendea unyama mlalamishi ambaye kwa miaka miwili sasa amekuwa akipokea matibabu katika hospitali na pia akipewa ushauri,” alisema Bi Kimilu.

Hakimu alisema Wangari alipata majeraha mabaya ya kiuno na hata itakuwa vigumu kujifungua kwa vile mfuko wa uzazi uliathirika kutokana na kishindo cha kuangukia vyuma na sakafu.

Wangari alipata majeraha hayo siku ya kwanza kukutana na Gatama katika afisi yake katika jumba la Ambank jijini Nairobi.

Akitoka nyumbani, Wangari alimweleza mama yake alikuwa anaenda kukutana na rafikiye jijini.

Lakini hakurudi nyumbani kwani alifurushwa kutoka orofa ya 12 alipokataa kukesha na mshtakiwa.

Alilala katika Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) kwa miezi mingi na sasa anatembea kwa msaada wa mkongojo.

Mshtakiwa alipewa siku 14 kukata rufaa.

  • Tags

You can share this post!

KIPWANI: Katoi wa Tabaka alivyosalia na ‘baby...

Wauzaji muguka washtaki kaunti

T L