Michezo

ATAHAMA? Bayern Munich tayari kumshawishi Roberto Firmino kuagana na Liverpool

February 11th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MUNICH, UJERUMANI

BAYERN Munich wako tayari kutoa kima cha Sh10.5 bilioni ili kumshawishi fowadi matata Roberto Firmino, 28, kuagana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu.

Chini ya mkufunzi Hans Flick, Bayern wamepania kujinasia huduma za nyota huyo mzaliwa wa Brazil kwa matarajio kwamba atakuwa kizibo kamili cha mvamizi Robert Lewandowski, 32. Lewandowski atabanduka uwanjani Allianz Arena mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

Katika mahojiano yake na wanahabari mwishoni mwa mechi ya Bundesliga iliyowakutanisha na RB Leipzig wikendi iliyopita, Flick alifichua pia maazimio ya kuhemea upya maarifa ya kiungo Leroy Sane wa Manchester City.

Sogora huyo raia wa Ujerumani alikuwa pua na mdomo kubanduka uwanjani Etihad mwanzoni mwa msimu huu ila akapata jeraha baya la goti ambalo limemsaza mkekani kwa kipindi kirefu. Ilikuwa hadi wiki iliyopita ambapo Sane, 24, alianza kushiriki mazoezi mepesi kambini mwa Man-City.

Hapana shaka kwamba ujio wa Firmino na Sane utawafanya Bayern kuwa miongoni mwa vikosi vinavyojivunia safu bora zaidi za mbele katika soka ya bara Ulaya.

Kwa misimu mitatu iliyopita, Firmino amekuwa tegemeo kubwa la Liverpool huku ushirikiano wake na Mohamed Salah na Sadio Mane ukiwezesha kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kujitwalia taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la Dunia na Uefa Super Cup katika kipindi cha miaka miwili.

Kufikia sasa, Liverpool wanahitaji kusajili ushindi katika mechi sita pekee kati ya 13 iliyosalia ili kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun nchini Uingereza, Liverpool wako radhi kukatiza uhusiano wao na Firmino ili wapate fursa ya kumsajili chipukizi Timo Werner, 23, ambaye kwa sasa ni mhimili mkubwa katika kikosi cha Leipzig, Ujerumani.

Ili kuweka hai matumaini ya kutetea ufalme wa EPL msimu ujao, Liverpool tayari wameanza mazungumzo ya kubaini mipango ya baadaye ya kila mmojawapo wa wachezaji wao kwa ushirikiano na mawakala wao.

Ingawa wengi wa nyota wa Liverpool hawana nia yoyote ya kubanduka uwanjani Anfield, huenda baadhi yao wakahiari kubanduka ili kujipa uhakika wa kuunga vikosi vya kwanza kambini mwa waajiri wao wapya.

Japo matamanio ya kocha Pep Guardiola yamekuwa ni kumdumisha Sane ugani Etihad, nyota huyo amewahi kufichua ukubwa wa kiu ya kutua Bayern baada ya kujipata akisugua benchi katika takriban kila mchuano kambini mwa Man-City.

Kiini cha Bayern kuziwania huduma za Sane ni ulazima wa kulijaza pengo la Philippe Coutinho ambaye anatazamiwa kuagana nao mwishoni mwa kipindi chake cha mkopo msimu huu.

Barcelona wako radhi kumtia Coutinho mnadani mwishoni mwa msimu huu na tayari maarifa yake yanamezewa mate na Manchester United, Chelsea na Tottenham Hotspur.

Mwishoni mwa wiki jana, Barcelona walitangaza bei mpya ya Coutinho kuwa Sh11 bilioni baada ya Bayern kushikilia kwamba hawana nia ya kumpokeza kiungo huyo mzaliwa wa Brazil mkataba wa kudumu mwishoni mwa muhula huu.

Coutinho, 27, anahusishwa pia na uwezekano wa kurejea kambini mwa Liverpool au kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) ambao wamekuwa wakimkeshea kwa kipindi kirefu.

Badala ya kumdumisha Coutinho kambini mwao kwa mkataba utakaogharimu zaidi ya Sh14 bilioni, Flick amewataka Bayern kujitwalia huduma za chipukizi Kai Havertz ambaye atakuwa radhi kuagana na Bayer Leverkusen kwa kima cha Sh6.5 bilioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Express nchini Uhispania, Barcelona ambao kwa sasa wananolewa na kocha Quique Setien, wanapanga pia kukatiza uhusiano wao na nyota Ousmane Dembele ili kujipatia fedha zikatazowawezesha kupata kizibo cha Luis Suarez.

Coutinho ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Inter Milan nchini Italia, alinunuliwa na Barcelona kutoka Liverpool kwa kima cha Sh19 bilioni mnamo Januari 2018.

Kufikia sasa, anajivunia kuwafungia Bayern mabao saba na kuchangia mengine manane kutokana na mechi 26 zilizopita za Bundesliga.

Coutinho hajafunga bao jingine tangu apachike wavuni magoli matatu katika mechi ya ligi iliyowakutanisha na Hertha Berlin mnamo Disemba 14, 2019.