Kimataifa

Atakayemuoa binti yangu bikira nitampa Sh24 milioni, bwanyenye atangaza

March 5th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

Chumphon, Thailand

BWANYENYE mmoja ameahidi kumtuza Sh24 milioni yeyote atakayemuoa bintiye bikira wa miaka 26,  kisha kumpa mali yake yote.

Bw Arnon Rodthong, 58 akimweka bintiye sokoni alisema kuwa ana uwezo wa kuzungumza kizungu, Kichina na ni bikira. Aidha, alisema kuwa bintiye Karnsita amekuwa akimsaidia katika biashara anayomiliki ya kiwanda cha matunda katika mkoa wa Chumphon, kusini mwa Thailand.

Bw Rodthong alisema japo utamaduni wa jamii nyingi nchini Thailand unaelekeza kuwa mwanamume alipe mahari kwa mwanamke, yeye atamwondolea atakayemwoa bintiye uhitaji wa kulipa mahari.

Badala yake, alisema kuwa atamlipa atakayemuoa Sh24 milioni, pamoja na shamba lake kwa jina Durian, lenye thamani mabilioni ya pesa.

Aliendelea kusema kuwa hakuna anayezuiliwa kutafuta mkono wa bintiye, iwe ni utaifa ama rangi, bora awe mume atakayetia bidii na amfurahishe motto huyo.

“Nataka mtu wa kuchunga biashara yangu na kuistawisha, sitaki mtu kwa kuwa ana shahada ama stashahada,” akasema.

Ijapokuwa ana watoto wengine, wakiwamo wa kiume na ambao wanaendesha biashara, mfanyabiashara huyo amesema kuwa punde bintiye akipata mume, atampa mali yake yote.

Shamba la Bw Rodthong la Durian husaga matunda tani 50 kila siku, likiwa kubwa Zaidi eneo hilo.

Bintiye naye alimtaka yeyote atakayemuoa kufahamu kuwa hata akipewa pesa hizo, itambidi ampeleke Korea kufanyiwa matibabu ya upasuaji wa kubadili ngozi ‘plastic surgery.’

“Ni kweli bado sina mpenzi, ikiwa nitaolewa na mtu, nataka awe mwenye bidii, mzuri na anayependa familia yake,”akasema Bi Rodthong.