Michezo

Atalanta yaduwaza Liverpool kwenye UEFA ugani Anfield

November 26th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

ATALANTA walifunga mabao mawili chini ya dakika nne za kipindi cha pili na kuwacharaza Liverpool 2-0 katika matokeo yaliyoacha wazi kampeni za Kundi D za kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kikosi cha Liverpool kilichojivunia mabadiliko mengi kilishindwa kuelekeza kombora lolote langoni pa Atalanta kwenye mchuano huo uliotandaziwa ugani Anfield mnamo Novemba 25, 2020.

Josip Ilicic aliwaweka Atalanta kifua mbele katika dakika ya 60 kabla ya Robin Gosens kufungia miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) goli la pili dakika nne baadaye.

Mohamed Salah aliyekuwa akirejea kambini mwa Liverpool kwa mara ya kwanza baada ya kukosa michuano mitatu iliyopita kwa sababu ya corona, alipoteza nafasi ya pekee aliyoipata katika dakika ya 71.

Pindi baada ya kufungwa bao la pili, kocha Jurgen Klopp wa Liverpool alifanya mabadiliko manne ya haraka kwa kuleta uwanjani Roberto Firmino, Diogo Jota, Andrew Robertson na Fabinho japo hatua yake hiyo haikuzaa matunda yoyote.

Kichapo ambacho Liverpool walipokezwa kilikuwa chao cha kwanza uwanjani Anfield tangu Septemba 2018.

Licha ya kipigwa, Liverpool bado wanasalia kileleni mwa Kundi D kwa alama tisa, mbili zaidi mbele ya Ajax na Atalanta. Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) sasa wanahitaji ushindi katika mchuano mmoja zaidi kati ya miwili ijayo dhidi ya Ajax na Midtjylland ili kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

Klopp alilaumu waratibu wa michuano ya EPL kwa kichapo hicho walichopokezwa na Atalanta akishikilia kwamba mrundiko wa mechi katika ratiba ya kipute hicho ulichangia idadi kubwa ya majeraha na uchovu.

Kukosekana kwa wanasoka kadhaa wa haiba kubwa kambini mwa Liverpool pia kulichangia kusuasua kwa kikosi cha Klopp kilichosalia kutegemea maarifa ya chipukizi Curtis Jones, Rhys Williams na Neco Williams.

Kuchezeshwa kwa makinda hao kulifanya Liverpool kuwa kikosi cha kwanza baada ya miaka 10 kuwahi kuwajibisha matineja watatu raia wa Uingereza katika mchuano mmoja wa UEFA.

Liverpool ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Brighton katika mechi ya EPL mnamo Novemba 28, 2020, walifanyia kikosi chao kilichoshinda Leicester City 3-0 mnamo Jumapili mabadiliko matano muhimu. Miamba hao watakuwa baadaye wenyeji wa Ajax mnamo Disemba 1, 2020 ugani Anfield kwa gozi la UEFA.

Miongoni mwa wansoka wa haiba waliokosa kuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool dhidi ya Atalanta kwa sababu ya majeraha ni Trent Alexander-Arnold, Joe Gomez, Virgil van Dijk, Jordan Henderson, Xherdan Shaqiri, Naby Keita, Thiago Alcantara na Alex Oxlade-Chamberlain.