Michezo

ATATUA ARSENAL? PSG, Juventus na Arsenal zang'ang'ania beki wa Real Madrid

July 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU ya Arsenal imeonyesha nia ya kumuwania beki wa pembeni Marcelo Silva wa Real Madrid ambaye pia anang’ang’aniwa na klabu nyingine kubwa za Ulaya.

Raia huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 31 ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa kutaka kuondoka Madrid baada ya kocha Zinedine Zidane kusajili Ferland Mendy kutoka Lyon kwa Sh7 bilioni.

Hata hivyo, Arsenal imejitoza kwenye vita hivyo ambapo itabidi wajitahidi mbele ya vigogo wa Paris Saint-Germain (PSG), Juventus na AC Milan ambazo tayari zimeanza mazungmzo na rais wa Madrid, Florentino Perez.

Marcelo anataka kuondoka baada ya kuichezea Madrid kwa kipindi cha miaka 13.

Arsenal ambayo pia imemuorodhesha Kieran Terney miongoni mwa wachezaji watakaosajiliwa, imetangaza mpango wa kuimarisha safu yao ya ulinzi.

Habari za mpango wa kumnasa Marcelo zimepokelewa kwa furaha na mashabiki wengi wa klabu hiyo wanaofikiria atakiongezea nguvu kikosi hicho cha kocha Unai Emery.

Marcelo amekuwa na ujuzi wa miaka 13 katika ngazi ya kimataifa kiasi cha wengi kumtambua kama beki bora wa upande wa kushoto.

Akiwa na Madrid, staa huyo amewasaidia kutwaa mataji manne ya La Liga, nne ya Klabu Bingwa barani Ulaya, mbali na mengine mbalimbali.

Beki huyo vilevile amewahi kujumuishwa katika kikosi bora cha FIFA mara nne, kikosi bora cha UEFA mara tatu na kikosi bora cha La Liga mara moja.

Kufuatia maombi kutoka kwa klabu mbalimbali, imebidi nyota huyo aanzishe mazungmzo na rais Florentino Perez ili akubaliwe kutafuta maisha mapya.

Kadhalika, Arsenal inajipanga kuwasilisha maombi kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji Wilfried Zaha wa Crystal Palace baada ya ombi la awali kukataliwa.

Arsenal ilitaka kumsajili nyota huyo kwa Sh6 bilioni, huku Palace wakitaka mara mbili ya kiasi hicho.

Sasa ripoti za hivi punde zimesema kwamba Arsenal wapo tayari kuongeza, lakini baada ya kuwapiga bei wachezaji wao kadhaa.

Kwa sasa, Zaha yumo nchini Misri kwenye michuano ya AFCON akiichezea Ivory Coast ambayo leo itakutana na Algeria katika hatua ya robo-fainali.

Manchester United

Wakati huo huo, Manchester United imeripotiwa kuwa mbioni kumpigania kiungo Bruno Fernandes wa Sporting Lisbon ya Ureno.

Habari zaidi kutoka kwa klabu hiyo ya Old Trafford zimesema kocha Ole Gunnar Solskajaer anataka nyota huyo ajaze pengo la Paul Pogba endapo ataondoka na kujiunga na Real Madrid kama inavyodaiwa.

Tayari United wameambiwa watoe Sh9 bilioni kumnasa kiungo huyo ambaye iwapo watamkosa, itabidi wafufue juhudi za kumwania Saul Niguez wa Athletico Madrid.

Kocha Ole Gunnar Solskajaer ameamua kukisuka kikosi chake baada ya timu hiyo kulemewa vibaya msimu ulipokuwa ikimalizika, ambapo alifanikiwa kushinda mechi mbili pekee kati ya 13.

Tayari Ander Herrera na Antony Valencia wameondoka, wakati huu Alexis Sanchez na Romelu Lukaku wakitarajiwa kuhama. Daniel James amekuwa mchezaji wa kwanza kujiunga na mabingwa hao wa zamani, huku wengine zaidi wakitarajiwa kuwasili.