Michezo

ATATUA UTURUKI? Maskauti wa Galatasaray watua London kutafuta huduma za Wanyama

August 14th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MASKAUTI wa kikosi cha Galatasaray Uturuki wametua jijini London, Uingereza kuanzisha mazungumzo yatakayomshuhudia kiungo Victor Wanyama akibanduka kambini mwa Tottenham Hotspur.

Kwa mujibu wa gazeti la Fanatik nchini Uturuki, ujumbe wa Galatasaray nchini Uingereza upo chini ya mkurugenzi wao wa soka Sukru Haznedar ambaye anatazamiwa kuwashawishi Tottenham kumwachilia nahodha huyu wa Harambee Stars kufikia Agosti 31, 2019.

Mbali na Wanyama, 28, Galatasaray wanapania pia kujinasia huduma za kiungo matata wa Chelsea, Tiemoue Bakayoko kabla ya muhula wa usajili miongoni mwa vikosi vya Ligi Kuu ya Uturuki kutamatika rasmi mwishoni mwa mwezi huu.

Kinachosubiriwa kwa sasa na usimamizi wa Galatarasay ni ripoti ya Haznedar ambaye katika mahojiano yake ya awali na Fanatik, alikariri kwamba dalili zote zinaashiria kwamba Spurs watakuwa radhi kuagana na Wanyama aliyewahi kuhusishwa pia na klabu za Fenerbahce, West Ham United na Bournemouth.

Mustakabali wa Wanyama jijini London umekuwa ukizingirwa na suitafahamu tele tangu wepesi wake wa kupata majeraha umpotezee uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Spurs chini ya mkufunzi Mauricio Pochettino.

Sogora huyu wa zamani wa Celtic na Southampton hakuwa sehemu ya kikosi cha Spurs kilichowapepeta Aston Villa 3-1 katika mchuano wao wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wikendi iliyopita.

Mkataba

Msimu jana, Wanyama ambaye angali na miaka miwili katika mkataba wake na Spurs alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Spurs mara nne pekee katika jumla ya michuano 13 aliyosakata.

Kikubwa zaidi ambacho kinatarajiwa kuchangia kuvunjika kwa ndoa kati ya Wanyama na Spurs ni ujio wa kiungo mkabaji Tanguy Ndombele aliyesajiliwa kwa kima cha Sh8.5 bilioni kutoka Olympique Lyon ya Ufaransa.

Fedha hizi zilizowekwa mezani na Spurs zilimfanya Ndombele kuwa mchezaji ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi hicho katika historia yake.

Pindi baada ya kurejea London Kaskazini kuungana na wenzake kambini mwa Tottenham mwishoni mwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON), Wanyama alipata jeraha la goti. Georges-Kevin Nkoudou ni mchezaji mwngine ambaye Tottenham imepania kumtia mnadani muhula huu.