Dondoo

Atemwa na demu kwa kutomlipia karo

August 8th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MUKONDE, MAKUENI

MWANADADA mmoja kutoka hapa aliwashangaza wenzake alipomtema mpenzi wake kwa kukataa kumlipia karo.

Inasemekana demu alikuwa katika chuo kikuu alipokutana na jamaa huyo na wakapendana.

Baada ya mwaka mmoja mapenzi kati ya wawili hao yalianza kunoga.

Ilifika wakati demu alipotatizika kulipa karo na akamuomba jamaa ampige jeki akamilishe masomo yake naye jamaa akakaidi agizo hilo.

Siku ya kioja demu alimualika jamaa chumbani na akamweleza hali ngumu aliyokuwa akipitia kupata karo. Kwa unyenyekevu alimuomba jamaa amsaidie kulipa karo ya shule naye jamaa akakaa ngumu.

“Beb, najua unanipenda na pia mimi ninakupenda ila nakuomba kitu kimoja. Sasa niko katika mwaka wa mwisho chuoni. Naomba unisaidie kulipa karo na baada ya kumaliza masomo tutaoana mara moja,” demu alimwambia jamaa.

Inasemekana jamaa alichemka na kuanza kumlaumu demu. “Hei, sasa umeanza kunipa majukumu na bado hatujaoana. Hapana, kama ulipanga mambo yako hivyo mimi siwezi na sina pesa za kukulipia karo,” jamaa alimwambia demu.

Jamaa alimfananisha kipusa na wengine wanaolipiwa karo na wapenzi wao na kisha kuwatema wakimaliza chuo.

Demu alimgeukia jamaa na kumzomea vikali.

“Gumegume wewe, kwa hivyo hauwezi kunisaidia na unadai unanipenda na ungependa kunioa. Kwa taarifa yako sasa nimejua haunipendi na kuanzia leo uhusiano wetu tumeuzika katika kaburi la sahau,” demu alimwambia jamaa.

Inasemekana baada ya kitumbua cha jamaa huyo kuingia mchanga alienda zake naye demu akaendelea kusukuma gurudumu la maisha bila kumshirikisha jamaa huyo. Hata hivyo haikujulikana demu ikiwa demu alifaulu kupaya karo.