Habari Mseto

Athari za El Nino Mukuru-Kayaba

January 15th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

ZAIDI ya familia 100 katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kayaba, South B zililazimika kuhama nyumba zao baada ya mafuriko kuvuruga maboma yao.

Vibanda vya kuendeshea biashara pia viliathirika kutokana na mvua kubwa iliyoshuhudiwa wikendi.

Akizungumza na Taifa Leo Dijitali, Jumatatu, Januari 15, 2024, naibu kamishna kaunti ndogo ya Starehe, Bw John Kisang alisema mvua kubwa iliyonyesha kuanzia Ijumaa hadi Jumalipi ilisababisha hasara zaidi katika maeneo kadha ndani ya eneobunge la Starehe.

Alisema katika eneo la Crescent na Budalangi, Mukuru-Kayaba, nyumba kadhaa zilisombwa na maji huku wakazi wakikadiria hasara kubwa baada ya vyombo na bidhaa zingine za kimsingi kubebwa na kuharibiwa.

Wenyeji walilazimika kuhamia maeneo salama kwa sababu ya athari za mafuriko.

Paipu iliyopitisha nyaya za stima yenye nguvu nyingi ilivyoinama kwenye Mto Ngong kufuatia athari za mafuriko Kayaba/Hazina, South B. PICHA|SAMMY KIMATU

Hali kama hiyo ilishuhudiwa katika mitaa mingine ya mabanda, ikiwemo Maasai Village, Mattress, Sokoni, Fuata Nyayo, Mariguini, Commercia, Kenya Wine, Kaberira na Sokoni.

Mitaa hiyo yote imo ndani ya tarafa ya South B.

Bw Kisang alidokeza kwamba shule mbili; ya msingi ya Race Course na ya Ainsworth, nyanja zake ziliharibiwa na mvua.

Katika eneobunge la Embakasi Kusini, nyumba na vibanda zilisombwa na maji kufuatia kupasuka kwa kingo za mto Ngong.

Hali kama hiyo vilevile ilishuhudiwa katika mitaa mingine ya mabanda ambapo nyumba hasikusazwa na maji katika tarafa ya Viwandani, Kaunti ndogo ya Makadara.

Bw Kisang alisema mtaa wa mabanda wa Kayaba, maji yaliangusha mti mkubwa karibu na daraja la Kayaba/Hazina huku mizizi ya mti huo ikisababisha nyumba ya orofa moja ya mabati kubomoka.

Mto Ngong mtaani Kayaba/Hazina, South B ulivyofurika. PICHA|SAMMY KIMATU

Kufuatia uharibifu huo, mafundi walikuwa mbioni kukarabati nyumba hiyo inayomilikiwa na ajuza.

Barabara kadha na kivukio cha magari na pikipiki cha Kayaba/Hazina, hazipitiki.

Hali kadhalika, paipu ya chuma ambayo imepitisha nyaya za stima zenye nguvu nyingi ilivunjika baada ya ng’ombe wawili waliosombwa na maji kugonga chuma hicho na kusababisha kuning’inia ndani ya mto huku nguzo zake za simiti zikipasuka.

Vyoo kadhaa na fanicha pia zilizombwa na mafuriko.

Huku ikifasiriwa El Nino inayoshuhudiwa maeneo mbalimbali nchini huenda ikaendelea hadi mwishoni mwa Januari 2024, wakazi wa mitaa ya mabadanda wametakiwa kuwa waangalifu na kuwa ange.