Athari za janga la Covid-19 zilisukuma wengi katika sekta ya kilimobiashara

Athari za janga la Covid-19 zilisukuma wengi katika sekta ya kilimobiashara

Na SAMMY WAWERU

WENGI wa walioathirika kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini waliingilia sekta ya kilimo na ufugaji.

Hata ingawa ni sekta ambayo haikuathirika kwa kiasi kikubwa, Ubalozi wa Kifalme wa Danish (RDE) hapa Kenya unasema imekuwa ikifanya vyema. Aidha, RDE imekuwa ikiendeleza miradi ya kilimo, kuinua kina mama, vijana na wakulima wenye mashamba madogo.

“Idadi kubwa ya watu imeingilia kilimo-biashara. Ingawa hata kabla ya Covid kutua nchini, sekta ya kilimo imekuwa ikifanya bora,” akasema Bw Charles Wasike, Afisa anayesimamia mikakati RDE, hasa kuangazia masuala ya kilimo na ufadhili wa bunifu kukabili mabadiliko ya tabianchi (climate change).

“Tukikagua na kutathmini takwimu, sekta ya kilimo haijaathiriki sana na mikumbo inayofika uchumi.” Alisema hayo wakati akihutubu jijini Nairobi, katika hafla iliyoandaliwa na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo.

Aidha, alisisitiza kwamba kujiri kwa virusi vya corona nchini, na ambavyo ni janga la kimataifa, hakukuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo, anayohoji imesalia ngangari. RDE chini ya Wizara ya Masuala ya Kigeni Denmark (Danida), inaendeleza mipango ya kuinua wakulima nchini.

Bw Charles Wasike, Afisa anayesimamia mikakati katika Ubalozi wa Kifalme wa Danish (RDE) hapa Kenya anasema sekta ya kilimo imesalia ngangari licha ya athari za corona…Picha/ SAMMY WAWERU.

“Lengo letu ni kusaidia kubuni nafasi za kazi, kuhimiza wakulima wakumbatie mifumo bora na salama kuzalisha chakula na kulinda mazingira,” Wasike akasema. Afisa huyo alisema miradi ya RDE inalenga sana vijana, kina mama na wakulima wa mashamba madogo.

Vijana wananufaika chini ya Ubalozi wa Kifalme wa Danish, kupitia makundi ya wale ambao hawajapata kisomo cha kutosha na waliohitimu mafunzo na taaluma mbalimbali vyuoni ila hawajapata ajira. “Maendeleo ya taifa yanajiri kupitia mikakati ya serikali, na tutaendelea kushika mkono Kenya,” akaahidi.

Bw Wasike alisisitizia haja ya wakulima kutilia maanani mifumo bora, ili kupata mazao salama. “Usalama wa chakula (akimaanisha kilichozalishwa bila kutumia pembejeo – fatalaiza na dawa zenye kemikali), ndio ufunguo wa lango la masoko yenye ushindani mkuu,” akafafanua.

“Tunapaswa kuzalisha chakula bora na salama, kiwe cha soko la humu nchini au la kimataifa,” akaongeza. Huku mabadiliko ya tabianchi yakizidi kuathiri hali ya anga na hewa, Wasike aidha alisema umewadia wakati kuendeleza shughuli za biashara na kilimo kwa njia ya kipekee, ili kudumisha mazingira.

“Tubadilishe mienendo yetu ya biashara, ili tuweze kukabili kero ya mabadiliko ya tabianchi.” Kauli ya afisa huyo wa RDE imejiri siku chache baada ya Kongamano la Kimataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP26, kufanyika Glasgow, Uingereza kati ya Oktoba 31 – Novemba 12, ambapo viongozi waliohudhuria waliahidi kukaza kamba mapambano dhidi ya athari zilizoibuka na zinazoendelea kujiri.

Rais Uhuru Kenyatta, ni kati ya viongozi waliohutubu katika mkutano huo, akiahidi “Kenya iko tayari na itajitolea mhanga kuhakikisha imeafikia kigezo cha zaidi ya asilimia 10 ya misitu na upanzi wa miti”.

You can share this post!

Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya...

MESPT inavyojituma kupiga jeki sekta ya kilimo nchini na...

T L