Habari Mseto

'Athena panapochimbwa mawe ni hatari'

December 9th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa kijiji cha Athena Juja, Kaunti ya Kiambu wanahofia maisha yao baada ya shimo la eneo la kuchimba mawe kuachwa wazi.

Wakazi hao walisema kando ya barabara ya Mibaoini, shimo la kina kirefu eneo la uchimbaji wa mawe ya ujenzi limeachwa wazi huku likiwa hatari kwa usalama.

“Sisi wakazi wa hapa Athena tunahofia maisha yetu na ya watoto wetu kwa sababu shimo hilo linaweza kusababisha hatari kubwa,” alisema John Kimani ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.

Alisema watoto wengi hucheza karibu na pahala hapo na kwa hivyo hali hiyo inawaweka katika hali ya wasiwasi.

Wakazi hao walisema wahuni hupata nafasi nzuri ya kupora wapitanjia hasa jioni na usiku.

“Hata watoto ambao wako katika likizo hupenda kubarizi karibu na pahala hapo. Tunatoa mwito kwa Kaunti ya Kiambu kufanya juhudi kuona ya kwamba wanaziba shimo hilo haraka iwezekanavyo,” alisema Kimani.

Wakazi hao walisema mvua ambayo inaendelea kunyesha ndiyo chanzo kikuu cha eneo hilo kuwa hatari zaidi.

“Hata wachimbaji wa mawe ambao kufanya kazi hapo wanapata wakati mgumu kwa sababu maji yamejaa maeneo hayo yote,” alisema Martin Gitau ambaye ni mkazi wa Athena.

Sasa wakazi wa kijiji cha Athena na Juja wameonywa kutokaribia hapo kwa sababu ni hatari kwa usalama.

Mwezi mmoja uliopita eneo la Ndarugu Juja, sehemu ya uchimbaji mawe iliporomoka ambapo dereva mmoja wa lori na wasaidizi wake wawili walipondwa na pande la jiwe na kufariki papo hapo.