Dondoo

Atimua dadake kwa kumvurugia mke

February 21st, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KAMOLO, TESO

KIZAAZAA kilizuka katika boma moja eneo hili baada ya polo kumfurusha dada yake kwa kuwa na tabia ya kumgombeza mkewe.

Kulingana na mdokezi, dada ya polo alikuwa ameolewa kijiji kilichopakana na kwao. Mara kwa mara, kipusa huyo alikuwa akifunga safari kwenda kwao kwa kisingizio kwamba alitaka kumuona mama yake mzazi.

Duru zinaarifu kipusa akifika kwao, alikuwa akifululiza hadi boma la ndugu yake akitafuta kosa lolote kutoka kwa mke wa polo nia yake ikiwa angalau amrushie tusi.

Siku ya tukio, kipusa alifika kwao na kufululiza hadi kwa ndugu yake na kuanza kumgombeza mkewe bila sababu.

Polo alipowasili, alimkuta mkewe akitiririkwa na machozi. “Dada yako amekuwa hapa. Amenitusi na kisha akanipa makataa ya siku mbili niwe nimeondoka hapa,” polo alielezwa na mkewe.

Inasemekana polo alifululiza hadi kwa nyumba ya mama yake na kumkuta dada yake akipiga gumzo na mamake.

“Shida yako ni gani! Mbona hutaki kutulia kwako. Una shida gani na mke wangu wewe!” polo alimkaripia dada yake.

Kipusa alibaki mdomo wazi. Polo aliendelea kumrushia matusi bila kujali. “Wewe ni kinyangarika cha aina gani. Nasikia humpi amani mumeo. Usilete kisirani chako kwangu,” polo alimkanya kipusa.

Hasira zilianza kumpanda kipusa. “Achana na zako. Mkeo kama hataki kufanya jinsi ninavyotaka mbona nisimuonye,” kipusa naye alimshtumu polo.

Polo alishindwa kujizuia. Alimkaribia dada yake akitaka kumzaba kofi. Polo alichomoa kiboko baada ya kuona dadake hakushtuka.

“Nimesema enda kwako haraka. Usionekane huku tena. Shetani wewe!” alimkaripia kipusa.