Dondoo

Atimuliwa kuishi na mume kwa kakake

August 28th, 2019 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

BOITO, BOMET

POLO wa hapa alimtimua dada yake na mumewe kwa kugeuza nyumba yake kuwa ya kufanyia mapenzi.?

Kulingana na mdaku, mrembo alikosana na mumewe miezi kadhaa iliyopita na akatorokea kwa wazazi kwani mumewe ni mkali kama simba na alihofia huenda akamdhuru.

Baada ya kukaa na wazazi kwa muda, mrembo alimuomba ndugu yake anayefanya kazi mbali amwachie boma lake amchungie.

“Kaka ya dada huyo huishi na familia katika mji wa mbali ambako anafanya kazi. Bwana huyo huacha boma lake la ushago bila mtu wa kulilinda na dada alipojitolea kukaa huko alifurahi sana na kumpa funguo,” mdaku aliarifu.

Mambo yalienda shwari kwa muda huku jamaa akishukuru dada yake mara kwa mara kwa kulitunza boma vizuri kwa niaba yake.

“Kila mara jamaa alipofika ushago alifurahi kuona mambo yakiwa sawa katika boma lake kwa kuwa dada alifyeka nyasi na kupalilia maua vizuri,” mdokezi akatusimulia.?Mwanadada aliapa kutorudi kwa mumewe akidai kufanya hivyo ni kama kujipeleka kwa mauti.

“Huyo mtu ana unyama ajabu. Hafurahi hata nikimfanyia mengi mazuri. Yake tu ni kelele ndani ya nyumba,” mwanadada alielezea ndugu yake masaibu yake.

Kaka alimsikitikia dada na kuahidi kumsaidia aanze maisha upya.? Hata hivyo, juzi jamaa alipata ripoti kuwa dada na mume wake wamerudiana na wanaishi katika nyumba yake badala ya mrembo kurudi kwa boma lake kule alikoolewa.

“Jamaa alifunga safari hadi nyumbani na alipofika alijionea maajabu kwani wawili hao walikuwa wamegeuza nyumba yake kuwa kwao.

Mara moja jamaa aliwatimua wawili hao akiteta kuwa walimkosea heshima,” mdokezi alisema.