Dondoo

Atisha kukausha asali Krismasi

December 24th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

MAILI NANE, ELDORET

Kizaazaa kilizuka kwenye ploti moja mtaani humu baada ya kipusa kumzomea polo kwa kukataa kumpeleka mashambani msimu huu wa sherehe za Krismasi.

Kulingana na mdokezi, kipusa alikasirika na akaapa kumnyima asali hadi mwaka mpya utakapobisha.

“Ploti nzima watu wameenda mashambani. Kwani sisi tunakaa hapa kufanya nini?” kipusa alimshambulia polo.

Inadaiwa jamaa alijitia hamnazo. “Unakataa kunipeleka kwenu kwani unanificha nini? Hata mimi utanijua vizuri,” kipusa alimuonya polo.

Penyenye zinasema tangu amuoe mrembo, jamaa hakuwa amempeleka kwao jambo ambalo lilikuwa likimsumbua mrembo sana.

Duru zinaarifu kwamba polo alikuwa akimhadaa mrembo kwamba hajaoa ilhali alikuwa na wake wawili nyumbani.

Inadaiwa polo aliogopa kumpeleka mrembo nyumbani kwa kuhofia vita vikali.

“Lazima nijipange vizuri ndiposa nikupeleke kwetu. Mambo hayafanywi kienyeji hivyo,” polo alimueleza kipusa.

Kipusa hakutaka kusikia lolote kutoka kwa polo ila ujumbe wa kupelekwa mashambani.

“Uliponioa ulipanga nini? Wewe unakaa mkora. Kwanzia leo usifikiri mambo yatakuwa rahisi kwako,” kipusa aliapa.

Ukali wa kipusa ulimshitua polo.

“Naona unaapa sana. Ni jambo gani unapanga kufanya?” polo alimuuliza kipusa.

Duru zinasema kipusa aliendelea kumzomea polo bila kuogopa lolote.

“Usifikirie mimi ni mjinga. Akili zako ni ndogo sana. Kuanzia leo sitakuwa nikikupakulia asali hadi mwaka huu ukamilike,” kipusa alitishia.

Inadaiwa polo aliamua kukimya kwa kuhofia kuaibishwa.

“Ipo siku nitajipeleka kwenu mwenyewe na nibaki huko,” kipusa alitisha.