Dondoo

Atisha kuwalaani wajukuu watundu kumuombea kifo

November 7th, 2018 1 min read

Na Victoria Nduva

Kyumbi, Machakos

NYANYA mmoja mtaani hapa ametisha kuwalaani wajukuu wake kwa kumuombea afe haraka ili wagawane mali yake aliyotafuta kwa udi na uvumba.

Inasemekana kwamba nyanya aliwalea wajukuu wake kwa shida baada ya wanawe kuaga dunia. Hata hivyo, badala ya kusoma na kufanya kazi, waligeukia matumizi ya mihadarati na ulevi kupindukia.

“Wana wa nyanya huyo waliaga dunia na kumwachia wajukuu wake wanne ambao sasa wamegeuka kero kwa kumtakia kifo ili wagawane mali yake ambayo kila mtu anajua alimwaga jasho si haba akitafuta,” alisema mdokezi.

Vijana hao wamekuwa wakizua fujo na kumkosesha ajuza huyu amani kwa kumwambia kuwa wangetaka afariki mapema ili warithi mali yake.

Kulingana na mdokezi, nyanya hulazimika kumwajiri jirani kumpikia akihofia kuwa wajukuu hao wanaweza kumuwekea sumu kwenye chakula chake.

“Mama huyo anajulikana kama mtu mwenye mali na wenyeji wa eneo hili. Alijiwekea akiba na kutafuta mali ambayo anaitumia kuishi maisha bora.

Ni mali hii ambayo wajukuu wake wanaimezea mate na kutamani Mola ampumzishe waitwae badala ya kutafuta yao,” alieleza mdokezi.

Mara kwa mara, vijana wamesikika wakipanga njama ya kutwaa mali hiyo lakini juhudi zao huwa zinagonga mwamba.

Hivi majuzi, nyanya aliwaita mbele ya watu wa familia na kuwaambia kuwa anafahamu huwa wanamtakia kifo ili warithi mali yake. Aliwaambia kuwa wasipobadilika, atawalaani na kwamba atahakikisha hawatarithi mali yake yoyote.

Kwa wakati huu, nyanya huyo anaishi chini ya ulinzi mkali wa jamaa zake ambao wamewaonya vijana hao kuwa watachukuliwa hatua wakimdhuru.