Atiwa mbaroni korti ikidumisha Ringera

Atiwa mbaroni korti ikidumisha Ringera

Na WAANDISHI WETU

RAIS WA Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) alikamatwa jana muda mfupi baada ya Mahakama kuu kukataa kusitisha kuteuliwa kwa kamati ya kusimamia kandanda na Waziri wa Michezo, Amina Mohamed.

Mwendwa alikamatwa na maafisa sita kutoka idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) na kuzuiliwa katika makao makuu ya DCI.Msemaji wa Polisi Bruno Shioso alithibitisha kukamatwa kwa Mwendwa ambaye majuzi afisi yake ilivunjiliwa mbali na Serikali kufutaia madai ya ufisadi.

FKF, Mwendwa na kinara wa shirikisho la kandanda Barry Otieno waliwasilisha kesi ya dharura kupinga kamati inayoongozwa na Jaji (mstaafu) Aaron Ringera izimwe kutekeleza majukumu yake.Akikataa kupiga kalamu kamati hiyo Jaji Hedwing Ong’udi, alisema harakati za kuzindua utendakazi wa kamati hiyo ulianza Oktoba 14, 2021.

“Kamati ya Ringera ilianza kazi Oktoba 14, 2021 na wale ambao hawakuridhika wangelishtaki wakati huo. Sasa siwezi kusitisha utendakazi wake,” Jaji Ong’undi aliamuru na kuagiza kesi hiyo isikizwe Novemba 23, 2021.

Katika kesi hiyo FKF imewashtaki Mohamed, Msajili wa Vyama vya Umma, Kamati ya Usimamizi wa FKF na Mwanasheria mkuu.Wakili Charles Njenga anayewakilisha FKF, Mwendwa na Otieno aliomba mahakama kuu isitishe utendakazi wa kamati hiyo ya Ringera, akidai Waziri Amina alikaidi sheria alipoiteua.

Njenga alieleza mahakama uteuzi wa kamati hiyo itakayomulika ubadhirifu wa pesa unakinzana na Katiba na sheria za usimamizi wa dimba nchini.Wakenya wanapoendelea kumpongeza Waziri wa Michezo Amina Mohamed kwa kuvunjilia mbali afisi ya Nick Mwendwa, kamati mpya ya kusimamia soka nchini ilianza rasmi kazi yake jana kwa kupiga marufuku ligi zote za juu ikiwemo Ligi Kuu ya Taifa FKF-PL).

Katika mkutano uliohudhuriwa na wanahabari jana, Kamati hiyo ya muda chini ya Jaji Mstaafu Aaron Ringera ilichukua hatua hiyo siku chake tu baada ya kupewa mamlaka na Waziri wa Michezo Amina Mohamed.

Akizungumza katika mkutano huo, Ringera aliwahakikishia washikaji dau wa soka nchini kwamba chini ya utawala wake masuala yote ya soka nchini yataendeshwa kitaaluma, huku juhudi mbalimbali zikifanya kwa lengo la kujaribu kurejesha hadhi ya mchezo huo.

Alitangaza kwamba shughuli yao ni pamoja na kusimamia mechi kati ya Harambee Stars na Rwanda itakayochezwa Jumatatu ugani Nyayo.“Kufuatia mkutano uliofanyika leo asubuhi, tulikubaliana kwa pamoja kupiga marufuku ligi kubwa za FKF-PL, FKF Supa Ligi ya Taifa (NSL), FKF Daraja la Kwanza, FKF Ligi Kuu ya Wanawake, FKF Daraja la Kwanza Wanawake, Daraja la Kwanza kwa muda wa wiki mbili.

”Kadhalika Ringera alisema kamati yake imechukua jukumu la kusimamia Harambee Stars baada ya afisi ya Mwendwa kuvunjwa na Serikali kufuatia mapendekezo ya Msajili ya Michezo Rose Wasike.

Mwendwa na kundi lake wamezuiliwa kuingia katika afisi za FKF huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufuatia madai kwamba kamati yake ilitumia vibaya pesa za umma.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa Congo Boys FC, Alamin Ahmed Abdalla amempongeza Waziri wa Michezo, Amina Mohamed kwa kuchukua uamuzi wa kuvunjilia mbali Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na kuchagua kamati itakayosimamia mambo ya mchezo huo.

HABARI ZA JOHN ASHIHUNDU, NA ABDULRAHMAN SHERIFF NA RICHARD MUNGUTI

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Wanasiasa wakome kudhalilisha IEBC...

Mzee Kama wa Kinyanjui ateuliwa kuwa msemaji wa jamii ya...

T L