Atletico Madrid waendeleza masaibu ya Barcelona na kumzidishia kocha Koeman presha ya kupigwa kalamu

Atletico Madrid waendeleza masaibu ya Barcelona na kumzidishia kocha Koeman presha ya kupigwa kalamu

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid, waliwafikia Real Madrid kileleni mwa jedwali mnamo Jumamosi baada ya kukomoa Barcelona 2-0 katika matokeo yanayomweka kocha Ronald Koeman pembamba zaidi uwanjani Camp Nou.

Thomas Lemar alifungia Atletico bao la kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Joao Felix pamoja na Luis Suarez aliyefunga la pili dhidi ya waajiri wake wa zamani. Antoine Griezmann pia aliwajibishwa dhidi ya Barcelona ambao ni waajiri wake wa zamani ila aliletwa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Barcelona kupoteza ligini muhula huu na sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 12, tano nyuma ya Atletico wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone.

Ingawa alama za Atletico zinawiana na zile za Real (17), Atletico wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na Real ya kocha Carlo Ancelotti.

Kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Atletico, Barcelona walikuwa wameshinda mechi tatu na kuambulia sare mara tatu kisha kupokezwa vichapo vya 3-0 kutoka kwa Bayern Munich na Benfica kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Msururu wa matokeo hayo duni yanamweka Koeman katika presha ya kupigwa kalamu huku mikoba ya Barcelona ikianza tayari kuhusishwa na wakufunzi Andrea Pirlo, Antonio Conte na Xavi Hernandez.

Ingawa walizidiwa ujanja na wenyeji wao Atletico, Barcelona walipata nafasi kadhaa za kufunga mabao kupitia Philippe Coutinho, Frenkie de Jong na Memphis Depay waliomwajibisha kipa Jan Oblak katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Barcelona kwa sasa wanaingia mapumziko ya wiki mbili ili kupisha mechi za kimataifa na wanatarajiwa kurejea ugani mnamo Oktoba 17 watakaposhuka dimbani kumenyana na Valencia kwenye La Liga uwanjani Camp Nou.

“Iko kazi kubwa ya kufanywa kambini mwa Barcelona. Lakini haiwezi kufanywa katika kipindi cha siku moja. Inatubidi kujitahidi kuwaaminisha zaidi chipukizi wetu na kusalia na matumaini kwamba mafowadi wetu veteran watapona majeraha hivi karibuni na kurejea ulingoni mwa matao ya juu,” akasema Koeman ambaye ni raia wa Uholanzi.

  • Tags

You can share this post!

Njama ya Uhuru kubomoa Ruto yafichuka

Juventus waponyoka na alama tatu katika gozi la Serie A...