Michezo

Atletico wamsajili Kondogbia kutoka Valencia awe kizibo cha Partey aliyetua Arsenal

November 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ATLETICO Madrid wamemsajili nyota wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Geoffrey Kondogbia kutoka kwa wapinzani wao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Valencia.

Kondogbia, 27, ametia saini mkataba wa miaka minne kambini mwa kikosi hicho kwa ada isiyojulikana.

Kusajiliwa kwake kulichochewa na haja ya Atletico kujaza pengo lililoachwa wazi na kiungo matata raia wa Ghana, Thomas Partey aliyeyoyomea Uingereza kuvalia jezi za Arsenal mnamo Oktoba 5, 2020.

Kwa mujibu wa kanuni za uhamisho wa wachezaji nchini Uhispania, Atletico walipewa siku 30 zaidi baada ya muhula rasmi wa kusajiliwa kwa wanasoka kufungwa ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Partey.

“Kondogbia ndiye mwanasoka ambaye tumehisi ataweza kuwa kizibo kamili cha Partey. Ana uwezo wa kutamba katika safu yoyote ya kati – kuwakaba wapinzani na hata kushambulia,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Atletico.

Kondogbia ambaye ni mzawa wa Ufaransa, aliwahi pia kuvalia jezi za Sevilla kabla ya kutua AS Monaco nchini Ufaransa na kuchezea Inter Milan ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Hadi alipoanza kuchezea timu ya taifa ya C.A.R mnamo 2018, Kondogbia alikuwa amewajibishwa na kikosi cha Ufaransa kwenye mechi za kirafiki mara tano.

Amewajibishwa na C.A.R mara tatu kufikia sasa.

Kondogbia alichezea C.A.R katika mechi tatu za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) na wakashindwa kunogesha kipute hicho kilichoandaliwa nchini Misri.