Michezo

Atletico wapiga RB Salzburg na kusonga mbele UEFA

December 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ATLETICO Madrid walifuzu kwa hatua ya mwondoano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kuwapokeza Red Bull Salzburg ya Austria kichapo cha 2-0 mnamo Disemba 9, 2020.

Mario Hermoso aliwaweka wageni Atletico uongozini katika dakika ya 39 kabla ya kuchangia bao la pili lililofumwa wavuni na Yannick Carrasco katika dakika ya 86.

Mergim Berishaw wa Salzburg alishuhudia fataki yake ya mwisho wa kipindi cha pili ikigonga mwamba wa lango la Atletico. Salzburg walishuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa na ulazima wa kushinda ili kujikatia tiketi ya kushiriki hatua ya mwondoano.

Ushindi wa Atletico ambao wanafunzwa na kocha raia wa Argentina, Diego Simeone, uliwawezesha miamba hao wa Uhispania kufuzu kwa hatua ya mwondoano wakishikilia nafasi ya pili kwa alama tisa nyuma ya Bayern waliomaliza kileleni kwa pointi 16. Salzburg walijizolea alama nne, moja zaidi kuliko Lokomotiv Moscow katika Kundi A.