Dondoo

Atorokea kwa wakwe kuhepa kipigo cha mke

March 10th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KABATI, MURANGA

Polo mmoja kutoka eneo hili aliwashangaza wengi alipotorokea kwa wakwe zake kukwepa kichapo cha mkewe.

Inasemekana polo aliamua kuchukua hatua hiyo mkewe alipotisha kumwadhibu. Siku ya tukio, polo aliwasili nyumbani kwake na kupata mkewe akiwa amefura kama mandazi.

“Habari za jioni mama boi?” polo alimsalimia mkewe.

Mkewe aliinuka na kuelekea alikokuwa jamaa.

“Unataka kujua habari zangu ndio ufanye nini. Tangu asubuhi sisi tumekaa njaa halafu unataka kujua habari zangu,” alimkaripia polo.

Polo alipigwa na butwaa kusikia maneno hayo.

“Kila siku huwa nakuambia saa zako za kufika kwa boma sizipite saa kumi na moja. Madharau ni ya nini mwanamume wewe,” mwanadada aliwaka.

Inasemekana kuwa jamaa alikinyamaza naye mrembo aliingia chumbani na kutoka na fimbo mkononi. “Unafika nyumbani sasa hivi, mikono ni mitupu, unataka nikukule,” mwanadada alifoka.

Polo aliamua kurudi nyuma kidogo huku akiwa mwangalifu zaidi.

“Leo lazima utaonja viboko vyangu na hakuna utakaponipeleka. Hata mamako akileta mchezo nitamuadhibu pia,” kipusa aliapa.

Penyenye zinasema jamaa alifululiza mbio hadi chumba cha kulala na alipochomoka nje, mkononi alikuwa amebeba shati na suruali.

“Kaa hapo peke yako. Iwapo utanitamani, njoo kwenu utanikuta huko,” polo alimueleza mkewe.

Inadaiwa mwanadada aliduwaa aliposikia maneno ya polo. “Umenisumbua sana. Badala ya kukufukuza, acha niende kwenu niishi na mamako,” jamaa alimueleza kipusa huku akienda.

Kipusa alimtahadharisha polo dhidi ya kukanyaga kwao.

“Pengine nitapata amani kwenu. Nimechoka nawe,” polo alifoka huku akienda. Haikubainika kilichotokea jamaa alipofika kwa wakwe zake usiku huo.