Michezo

ATUA SPURS: Mourinho ndiye kocha mpya wa Tottenham

November 21st, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

TOTTENHAM Hotspur imetangaza kuteuliwa kwa Jose Mourinho kama kocha mpya wa klabu hiyo ambayo ilimtimua Mauricio Pochettino, Jumanne.

Mourinho anaongeza Spurs kwa orodha ya klabu alizowahi kunoa hapo awali zikiwemo FC Porto, Inter Milan, Chelsea, Real Madrid na Manchester United.

Kazi hii ni ya kwanza kwa Mreno huyo tangu apigwe kalamu na Manchester United mwishoni mwa mwaka 2018.

“Najivunia kujiunga na klabu hii inayojivunia historia refu na mashabiki sugu,” alisema kwenye taarifa yake kupitia kwa mtandao wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (EPL).

Akaongeza: “Ubora wa kikosi pamoja na wachezaji wa chuo cha kunoa vipaji unanipendeza. Kinachonivutia zaidi kufanya kazi na wachezaji hawa.”

Daniel Levy, mwenyekiti wa klabu, alisema: “Mourinho ni miongoni mwa makocha bora duniani. Ana ujuzi wa kutosha, anaweza kuwa kielelezo bora kwa timu na pia ni kocha mzuri. Amesaidia timu nyingi kutwaa mataji popote alikokuwa. Tunaamini kwamba ataleta nguvu mpya na imani tele miongoni mwa wachezaji.”

Mourinho ambaye alielezwa mtandaoni kuwa miongoni mwa makocha bora, ameshinda mataji 25, yakiwemo manne akiwa na timu nne za mataifa tofauti. Kadhalika ameshinda Ligi ya Klabu Bingwa barani mara mbili akiwa na FC Porto nchini Ureno na Inter Milan ya Italia.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 56 aliisaidia Chelsea kutwaa ubingwa wa EPL mara tatu alipokuwa na timu hiyo kwa mara mbili tofauti kabla ya kurejea nchini Uingereza mnamo 2016 kuinoa Manchester United.

Matokeo duni

Alitimuliwa mwaka 2018 kufuatia matokeo duni na amekuwa nje tangu wakati huo, wakati huo akifanya kazi ya uchambuzi kupitia Sky Sports.

Pochettino amefutwa kazi baada ya kukaa na Spurs kwa miaka mitano unusu, miezi michache tu baada ya kuiongoza Spurs kutinga fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya. Kwa sasa, Spurs wanashikilia nafasi ya 14 ligini kutokana na mechi 12.

Max Allegri aliyekuwa na Juventus pamoja kocha Eddie Howe wa Bournemouth pia walihusishwa na kazi hiyo.

Mourinho ambaye mechi yake ya kwanza itakuwa dhidi ya West Ham United ugenini aliripotiwa kukataa kazi kadhaa za kuandaa timu nchini China, Uhispania na nchini kwao Ureno, tangu afukuzwe Old Trafford.