Makala

Atumia alizeti kutatua migogoro kati ya wanyamapori na binadamu

December 16th, 2019 2 min read

Na MAGDALENE WANJA

ALIBANDIKWA jina “mwanamaji wa Tsavo” kutokana na juhudi zake za kuwachotea maji wanyama katika Mbuga ya Tsavo ili kuokoa maisha yao wakati wa kiangazi.

Mnamo mwaka 2016, juhudi za Bw Patrick Kilonzo zilivutia ulimwengu na kumletea sifa tele.

“Niliamua kujitolea kuwachotea maji wanyama hao baada ya mvua kukosekana kwa muda wa miaka miwili katika eneo hilo na kinyume na wanadamu ambao wanaweza kuitisha msaada, wanyama waliendelea kuteseka,” akasema Bw Kilonzo.

Ata hivyo, Bw Kilonzo alikuwa anapitia wakati mgumu kwani alikuwa na ugonjwa wa figo ambao ulikuwa ukimsumbua.

Changamoto hii haikumzuia kutekeleza wajibu wake wa kuwahudumia wanyama pori waliokuwa na kiu kutokana na hali ya ukame.

Mnamo Julai 2019, alipata ufadhili kutoka kwa kampuni ya Maithri Aquatech Private Limited ambao walikuwa tayari kumlipia matibabu yake nchini India ili kuwekwa figo nyingine.

Ata hivyo, baada ya kusafiri, matibabu hayo hayakufanyika kwani figo aliyofaa kupokea kutoka kwa nduguye ilikuwa haina nguvu inayohitajika katika mwili wake kwani ilikuwa dhaifu.

Bw Kilonzo alirejea nyumbani na anatarajiwa kupokea matibabu hayo punde atakapopata mtu wa kumpa figo nyingine.

“Punde tu matayarisho ya kupata figo nyingine yatakapokamilika, nitasafiri tena ili kupokea matibabu,” akasema Bw Kilonzo.

Licha ya hayo yote, Bw Kilonzo hajakata tamaa na mapenzi yake kwa wanyama pori yamemsukuma kufanya miradi zaidi ili kuwahifadhi.

Katika mradi wake wa hivi punde, anafanya ukulima ambapo anakuza alizeti kama mojawapo ya njia za kuzuia migogoro kati ya wanyamapori na binadamu wanaoishi karibu na mbuga.

“Nilianzisha mradi huu baada ya kuona vile ndovu wanaharibu mimiea ya wakulima katika eneo hili. Baada ya kufanya utafiti niligundua kwamba ndovu hawali alizeti na hivyo wakulima wanaweza kupanda mimea hii na baada ya kuvuna wanaweza kuuza na kununua chakula wanachotaka,” akasema Bw Kilonzo.

“Wakulima wengi katika sehemu zilizo karibu na mbuga husalia bila mapato baada ya kuliwa na wanyama kama vile ndovu,” aliongeza.

Alisema kuwa mradi huo tayari unazaa matunda kwani wakulima wengi sasa wana mapato mazuri kando na hapo awali.

“Tangu nilipoanza kulima mimea hii, ndovu wamevamia shamba langu mara nne na hawajakula hata mmea mmoja,” alisema Bw Kilonzo.

“Kando na kuuza mazao yake, alizeti huwavutia nyuki ambao wanatengeneza asali na hivyo basi wakulima wanaweza pia kufaidika kutokana na ufugaji wa nyuki,” aliongeza Bw Kilonzo.

Alisema kuwa wazo la kukuza alizeti lilimjia baada ya kuwaza kwa muda mrefu huku akiongeza kuwa ukulima huo unaweza kuwasaidia watu katika sehemu mablimbali nchini kwa kuzuia mizozo kati ya wanyama na binadamu.

Alisema kuwa mradi huo ambao ulianza mwezi Oktoba unategemea maji ya mvua kama mimea mingine shambani na hivyo haitawagharimu wakulima katika kunyunyizia mimea hio.

Alidokeza kuwa tayari kampuni ya Bidco imeanza kununua nafaka hiyo kwa wakulima ambao wanakuza tayari.

Kampuni ya Maithri Aquatech Private Limited pia imempa Bw Kilonzo mashine ya kisasa ambayo inaweza kukusanya maji kutoka hewani.

Mashine hiyo ilinunuliwa kwa Sh 1.7 milioni na ina uwezo wa kupata lita 1000 za maji kila siku.

“Mashine hiyo itawafaa sana wanyama haswa wakati wa kiangazi kwani maji yake ni safi na inaweza kutumika wakati wowote,” alisema Bw Kilonzo.

Mashine hiyo  tayari ishawasili katika bandari ya Mombasa. Bw Kilonzo alisema kuwa mashine hiyo itawekwa katika Mbuga ya Tsavo Mashariki ili kuwafaidi wanyama.

Bw Kilonzo alipewa Tuzo ya Rais kwa juhudi zake za kuwasaidia wanyama pori ambayo alipokea mwezi Julai kutoka kwa waziri wa utalii na wanyamapori, Bw Najib Balala.

Waziri Balala pia alidokeza kuwa baada ya matibabu ya Bw Kilonzo kukamilika, serikali itampa kazi kama Honorary Warden, kama njia ya kumtuza kutokana na juhudi zake.

Bw Balala alisema kuwa zaidi ya ndovu 440 walifariki mnamo mwaka 2017 kutokamna na ukame na serikali imeweka juhudi za kuwaokoa wanyama hao.