Habari Mseto

Atumia siku yake ya kuzaliwa kusaidia wakongwe

April 16th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

MWANAMUME mmoja Kaunti ya Lamu amegusa mioyo ya wengi pale alipotumia siku yake ya kuzaliwa kuzuru vijiji mbalimbali eneo hilo kugawanyia wakongwe barakoa, sabuni za maji na msaada wa chakula.

Francis Mugo, 27, ambaye ni afisa mtendaji wa Muungano wa Vijana na Mageuzi eneo la Pwani, alitumia muda wote wa siku yake ya kuzaliwa kwa njia ya kipekee pale alipowazuru wazee wa kati ya miaka 70 na zaidi vijijini mwao na kuwapa zawadi hizo na pia kuwapokeza mafunzo maalum ya kuwawezesha kuepuka kuambukizwa maradhi ya Covid-19.

Zaidi ya wazee 100 kutoka vijiji vya Mkunumbi, Mapenya, Hongwe, Bahari na Telelani walinufaika na msaada huo wa Bw Mugo.

Katika mahojiano na Taifa Leo muda mfupi baada ya kukabidhi zawadi wazee hao vijijini, Bw Mugo alisema umamuzi wake ulisukumwa na tafiti kwamba wazee ndio ambao wako katika hatari zaidi ya kupata Coronavirus na hata kupoteza maisha yao ikizingatiwa kuwa kinga yao ya mwili iko chini kufuatia umri wao mkubwa.

Bw Mugo pia alisema wazee wengi wamekuwa wakiugua maradhi, ikiwemo kisukari, msukumo wa damu na hata kansa, hatua ambayo inawaweka kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa Covid-19.

Alisema aliafikia kutumia siku yake ya kuzaliwa kutangamana na wazee katika jamii ili kuwasaidia kwa barakoa, sabuni za maji pamoja na vyakula ili kujikimu wakati huu mgumu ambapo uchumi umeharibika kutokana na mkurupuko wa Coronavirus nchini na ulimwenguni kwa jumla.

“Huku nikisherehekea siku yangu ya kuzaliwa, nimeafikia kuwafikia wakongwe katika jamii zetu, hasa wale wa miaka 70 kwenda juu. Nikishirikiana na wenzangu tulioandamana nao, tumewakabidhi wazee hao maski na pia kuwafunza jinsi ya kutumia maski hizo. Pia tumewapa sabuni na vifaa vingine vya kudhibiti usafi msimu huu wa janga la Corona. Isitoshe, tumewapa misaada ya chakula, ikiwemo ungawa mahindi, ngano, mchele na mafuta ya kupikia ili pia wajihisi kuthaminiwa katika jamii,” akasema Bw Mugo.

Aliwahimiza vijana eneo la Lamu na nchini kwa jumla kukoma kuwatelekeza wakongwe na badala yake kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia, ikiwemo kwa chakula, mavazi na hata kutunza afya zao.

Baadhi ya wazee waliozungumza na Taifa Leo muda mfupi baada ya kupokezwa zawadi hiyo hawakuficha furaha yao.

Mzee Kamande, 80, ambaye anaishi na ulemavu kijijini Mapenya, alimshukuru Bw Mugo kwa kujitolea kwake na kuwakumbuka wazee msimu huu wa Covid-19.

“Tunamshukuru Bw Mugo kwa juhudi zake. Ametufikishia misaada ya chakula, sabuni na barakoa za kujikinga dhidi ya Covid-19. Hatua yake yafaa kuigwa na wengi, ikiwemo viongozi wetu wa kisiasa eneo hili,” akasema Bw Kamande.

Bi Anne Wanjiku aliwashauri wazazi kuwafunza watoto wao kuwa na moyo wa kusaidia kama ule wa Mugo.

Alisema vijana wengi, ikiwemo wale walioko uongozini wamekuwa wachoyo ilhali wengine wakiwatelekeza wazee katika jamii.