Dondoo

Atupa mke kwa kuchoshwa na wakwe

April 30th, 2019 1 min read

Na John Musyoki

Kiritiri, EMBU 

JOMBI mmoja kutoka eneo hili aliwashangaza wazazi wake alipoamua kumtaliki mkewe akidai wakwe zake ni wasumbufu.

Penyenye za mtaani zinasema kalameni alidai wakwe zake walikuwa wakimtia presha kwa kukosa kuhudhuria harambee waliyoandaa na kutoa mchango wake.

Duru zinasema jamaa aliposusia harambee wakwe walimtisha na kumsuta vikali.

“Mimi nimechoshwa na tabia ya wakwe zangu. Nilipokosa kuhudhuria harambee ya kuchangisha pesa sasa wameeneza udaku kila mahali kunihusu. Sitaki mchezo na wakinichokoza nitampa binti yao talaka,” jamaa alisikika akiwaambia wazazi wake.

Jamaa alizidi kulalamika huku akidai kwamba wakwe zake walikuwa wakimtumia vibaya.

“Nimekasirika sana. Nililipa mahari yote na bado wazazi wako wananifuata waninyonye kila kitu. Wazazi wako wamekuwa wakiniharibia jina langu kila mahali. Hata hawana shukrani kwa kuwalipa mahari chungu nzima. Wakicheza na mimi nitakupa talaka uende ukaishi na wao huko kwenu,” jamaa alimgeukia mkewe na kumfokea.

Inasemekana jamaa aliwapigia wakwe zake simu na kuwakemea kwa kumtisha na kumkosea heshima mtaani. Hata baada ya wazazi wake kumtuliza jamaa aliwaka zaidi.

“Mimi sitaki kisirani. Nitampa mke wangu talaka. Kuishi maisha ya ukapera si hoja kwangu. Ni bora kuliko kuishi na wakwe wanaonikosesha usingizi,” jamaa alisema. Jombi huyo alizidi kuwaka huku watu wakimsihi atulie lakini dua zao ziliambulia patupu.

Ilibidi wazazi wake wafunge safari kwenda kwa wakwe zake ili kujaribu kutatua mzozo huo kwa sababu walikuwa wakimpenda mkaza mwana wao sana. Hata hivyo haikujulikana kilichojiri baada ya wazazi kutoka pande zote mbili kukutana.