Habari Mseto

Atupwa ndani kwa kujigamba kuwa gaidi sugu

September 5th, 2020 1 min read

Na TITUS OMINDE

MWANAMUME aliyejigamba kuwa gaidi na kukiri mashtaka mawili ya kujifanya afisa wa polisi na kughushi cheti cha tabia njema, amefungwa jela miaka mitatu na mahakama ya Eldoret.

Mnamo Agosti 31, Mathew Kiplangat Ng’eno, maarufu kama Jamal Mohammed, alikiri kosa la kughushi stakabadhi za polisi kwa kujifanya afisa wa polisi kutoka kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI.

Alipofika mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Eldoret, Bi Emily Kigen, mshtakiwa alikiri kosa la kughushi stakabadhi husika.

Upande wa mashtaka uliiambia korti kuwa, mshtakiwa ana rekodi ya uhalifu ikiwa ni pamoja na wizi ambapo mahakama kuu ilikuwa imemwondolea kifungo cha maisha baaada ya kukata rufaa dhidi ya kifungo husika.

Mahakama iliambiwa kuwa, mnamo Mei 22 alipatikana akighushi cheti cha tabia nzuri kinachodaiwa kutolewa na huduma ya polisi ya Kitaifa kupitia Afisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI).

Shtaka lingine lilisema mshtakiwa pamoja na wengine ambao hawakuwa kortini alipatikana akimiliki cheti cha tabia njema kikiwa na jina lake akidai alipokea kutoka kwa huduma ya polisi nchini.

Mtuhumiwa alifikishwa katika korti ya Eldoret kwa sababu ya mashtaka mengine ya ugaidi. Kesi hiyo itatajwa Septemba 24.