Habari Mseto

Atupwa ndani kwa kukataa kuhesabiwa, 3 wakamatwa

August 28th, 2019 1 min read

NA WAANDISHI WETU

MWANAMUME amefungwa miezi sita gerezani kwa kuzuia afisa wa sensa kumhesabu. Abraham Cheruiyot kutoka Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu alihukumiwa katika mahakama ya Eldoret Jumamosi.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, watu watatu walikamatwa katika lokesheni ya Kathangacini, kaunti ndogo ya Tharaka Kaskazini kwa kukataa kuhesabiwa kutokana na imani yao ya kidini.

Watatu hao ni wa dhehebu la Kabonokia na wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Marimanti baada ya kutoroka boma lao wakisema dini yao haiwaruhusu kushiriki mambo ya dunia kama sensa.

Dhehebu la Kabonokia pia limekataza waumini wake kwenda shuleni au kutibiwa hospitalini.

Katika kijiji hicho hicho, mwanaume mwingine alikamatwa baada ya kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba angewakatakata maafisa wa sensa iwapo wangefika kwake kutokana na machungu ya kukosa kupewa kazi hiyo ya kuhesabu watu.

Katika Kaunti ya Homa Bay, mwanaume alimuua nduguye ambaye alirejea nyumbani kuhesabiwa kufuatia mzozo wa ardhi.

Marehemu Joseph Olale, 56, alirejea nyumbani kwao katika kijiji cha Kamato Punde, wadi ya Lambwe kutoka mji wa Ahero anakofanya kazi ili ahesabiwe, lakini wakashiriki ugomvi na kakake kuhusu shamba la familia ndipo akauawa.

Kamanda wa polisi eneo hilo Charles Mwangi alisema mnshukiwa amekamatwa.

Katika Kaunti ya Vihiga, mwanaume alikamatwa Jumanne jioni baada ya kupanda juu mti asihesabiwa na maafisa wa sensa.

Bw Elias Asige kutoka kijiji cha Itumbi, lokesheni ndogo ya Givogi anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Serem huku mwanamke ambaye alipatikana kwenye boma lake bado akiandamwa na polisi baada ya kutoroka.

Kamishina wa Vihiga, Sammy Waweru alithibitisha kisa hicho na kusema maafisa wake wanamsaka mama aliyetoweka.

Ripoti za Alex Njeru, George Odiwuor, Derick Luvega na Titus Ominde