Dondoo

Atwangwa na mke kumsingizia ufuska

November 21st, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kakamega

Kizaazaa kilizuka hapa baada ya polo kupewa kichapo kwa kudai mkewe na shemejiye wana uhusiano wa kimapenzi.

Duru zinasema ndugu ya jamaa aliposikia madai ya polo, aliamua kumweleza yule mama. “Huyu bwana yako ana shida gan? Anafikiria mimi siwezi kutafuta mrembo ndio nidoee mkewe!” ndugu ya polo alichemka.

Inadaiwa mwanadada alimshauri shemeji yake waandamane ili wamuonye polo.

Walipofika kwa polo, wawili hawa waliungana na kuanza kumkemea. “Nimesikia umeniharibia jina sana. Mimi simtongozi mkeo. Na kama utaendelea na hayo madai yako walahi nitakuadhibu,” polo alionywa.

Inasemekana polo alirudia tena kauli yake. “Wewe umeonekana ukitembea na mke wangu. Unafanya nini na yeye?” polo aliuliza.

Maneno hayo hayakumfurahisha kakake na mkewe huyo. Wawili hao waliamua kwa pamoja kumnyorosha polo. “Hata mimi nimechoka na wewe. Umenizoea sana,” kipusa alisema huku akimuangushia mumewe kofi.

Kwa upande wake, ndugu ya polo aliendelea kumtandika ndugu yake bila huruma. “Hiyo bangi uliyovuta lazima iishe leo,” polo alimwambia nduguye.

Duru zinasema polo aliomba msamaha huku akiapa kutorudia tena lakini waliendelea kumuadhibu.

“Kama umeshindwa na majukumu yako kama mwanaume sema. Lakini kunisingizia maneno eti namtaka mkeo huo ni upuzi na ukome, sina haja naye kabisa,” polo alifoka.

Iliwabidi majirani kuingilia kati na kumuokoa lakini nao pia walimuonya akome kusingizia watu mambo yasiyo ya ukweli.