Atwoli, Oparanya wakagua Bukhungu matayarisho ya mkutano mkubwa wa kijamii yakikamilika

Atwoli, Oparanya wakagua Bukhungu matayarisho ya mkutano mkubwa wa kijamii yakikamilika

Na SHABAN MAKOKHA

MIPANGO ya kumtawaza Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya kama Msemaji wa wakazi wa Magharibi inaendelea kukamilika, hafla hiyo ikitarajiwa itafanyika katika uga wa Bukhungu mnamo Disemba 31.

Mkutano huo mkubwa utampa Bw Oparanya wadhifa huo ambao umekuwa ukishikiliwa na Kinara wa ANC Musalia Mudavadi aliyetawazwa kwenye hafla kubwa iliyoandaliwa uga huo huo mnamo 2016.

Kutokana na utafiti uliofanywa mwaka huo na kudhaminiwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Francis Atwoli, Mudavadi aliibuka wa kwanza akifuatwa na Bw Oparanya kwenye nafasi ya pili kisha Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula akaibuka nambari tatu.

Bw Atwoli anayedhamini mkutano wa mwaka huu pia, Jumatatu amewaongoza wabunge wa eneo hilo kutembelea uga huo kabla ya mkutano huo kuandaliwa siku ya mwisho wa mwaka huu 2021.

Kinara wa ODM Raila Odinga ambaye alimtembelea Bw Atwoli nyumbani kwake eneobunge la Khwisero, Jumapili, alikubali mwaliko kuwa ahudhurie mkutano huo ambao pia utakuwa wa Azimio la Umoja, ukanda wa Magharibi mwa nchi.

“Nimekubali mwaliko na nitahudhuria mkutano huo kwa sababu hapa ni nyumbani kwangu. Nawaomba watu wangu wajihami kwa silaha ambazo ni kura na kitambulisho ili mnipigie kura niwe rais wa tano wa Kenya,” akasema Bw Odinga akihutubia umati nje ya boma la Bw Atwoli.

Kando na Mabw Atwoli na Oparanya, wanasiasa wengine ambao wameukagua uga wa Bukhungu ambako maandalizi hayo yanaendelea ni Eseli Simiyu (Tongareni), Bernard Shinali (Ikolomani), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Raphael Wanjala (Budalang’i), Godfrey Osotsi (mbunge maalum), Justus Kizito (Shinyalu) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda.

“Baada ya mkutano huo, sisi kama wakazi wa eneo hili tutasonga mbele tukiwa kwenye mwelekeo unaoeleweka kisiasa,” akasema Bw Oparanya.

Wanasiasa wandani wa Bw Odinga waliokagua jinsi maandalizi yanavyoendelea ugani Bukhungu wamesema kuwa hakutakuwa na mkutano wowote eneo hilo kando na huo wa Bukhungu.

“Yeyote ambaye anajiona ni mwanaume athubutu kuandaa mkutano mwingine. Nimeweka mikakati yote ya kiusalama mjini Kakamega mnamo Disemba 31,” akaonya Bw Atwoli.

Kauli yake inajiri baada ya Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kutishia kuvuruga mkutano wa Bukhungu, akidai kuwa Mabw Mudavadi na Wetang’ula hawakuwa ‘wameshauriwa’.

Akizungumza wakati wa kuadhimisha tamaduni ya jamii ya Maragoli mjini Mbale, Kaunti ya Vihiga, Bw Malala alitangaza kuwa mkutano wa Bukhungu hautaendelea kwa sababu haujaidhinishwa na Bw Mudavadi.

“Mudavadi amethibitisha kuwa hatakuwa akihudhuria mkutano wa Bukhungu. Ningependa kuwaarifu wanaoratibu mkutano huo kuwa lazima wapate idhini ya Bw Mudavadi la sivyo mkutano huo hautaendelea kwenye ngome yangu ya kisiasa,” akasema Bw Malala.

Hata hivyo, alimwonya Bw Malala akisiema yeye ni mwanasiasa ambaye bado hajakomaa kisiasa na hafai kuwaelekeza visivyo watu wa Magharibi.

“Mimi ndiye nilimfanya Malala kuwa seneta na nina uwezo wa kumpokonya wadhifa huo. Mkutano wetu utaendelea na hawezi kuusimamisha,” akasema Bw Atwoli.

Bw Osotsi naye alidai seneta huyo ni kibaraka wa Naibu Rais Dkt William Ruto ndani ya ANC na amekuwa akifadhiliwa na mrengo wa UDA.

You can share this post!

Lusaka awarai wanasiasa Waluhya wasibuni vyama vingine

NMS haijamaliza miradi ikisalia miezi 3 pekee

T L