HabariSiasa

Atwoli sasa amsamehe Mudavadi kwa kuhepa kiapo cha Raila

February 19th, 2018 2 min read

Na SHABAN MAKOKHA

Kifupi:

  • Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya bila kutatizwa na yeyote
  • Bw Atwoli alikuwa ametaja Bw Mudavadi kuwa mwoga na kuomba msamaha
  • Bw Mudavadi anaweza tu kupokonywa wadhifa wa msemaji wa jamii na watu milioni moja Waluhya waliomuidhinisha   

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Bw Francis Atwoli, Jumapili alisema kwamba amemsamehe kinara mwenza wa NASA, Musalia Mudavadi, kwa kuhepa hafla ya kumuapisha kiongozi wa muungano huo Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018.

Bw Atwoli alitangaza hayo baada ya kukutana faraghani na Bw Mudavadi nyumbani kwake Khiswero, katika Kaunti ya Kakamega.

“Tumekubaliana kwamba Bw Mudavadi ataendelea kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya bila kutatizwa na yeyote,” alisema Bw Atwoli.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa kisiasa na wazee wa jamii ya Waluhya.

Bw Atwoli alikuwa ametaja Bw Mudavadi kuwa mwoga na kuomba msamaha jamii ya Waluhya kwa kumuidhinisha kuwa msemaji wao kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Bw Francis Atwoli alimwomba radhi Bw Musalia Mudavadi katika kikao cha faragha nyumbani kwake Khiswero, katika Kaunti ya Kakamega Februari 18, 2018. Picha/ Maktaba

Ni wazee kutoka kaunti tano za uliokuwa mkoa wa Magharibi ambao walisaidia kupatanisha Bw Atwoli na Bw Mudavadi baada ya tofauti kuzuka kiongozi huyo wa chama cha Amani National Congress (ANC) alipokosa kuhudhuria uapisho wa Bw Odinga.

 

Watu milioni moja

Baada ya mkutano wa Jumapili, Bw Atwoli alisema kwamba Bw Mudavadi anaweza tu kupokonywa wadhifa wa msemaji wa jamii hiyo na watu milioni moja kutoka jamii ya Waluhya waliomuidhinisha.

Alisema umoja ambao jamii iliasisi Desemba 31, 2016 unapaswa kulindwa kwa hali na mali.

Mwenyekiti wa wazee wa eneo la Magharibi ya Kenya, Bw Philip Masinde, alisema kwa kuungana, eneo hilo litafaulu kisiasa na kiuchumi.

Bw Mudavadi alimpongeza Bw Atwoli kwa kumkosoa alipokosa kuhudhuria hafla ya Januari 30 2018 katika bustani ya Uhuru Park.

“Ninapenda kukosolewa kwa sababu kunanifanya kufahamu ninapokosea,” alisema.

 

Umoja

Aliwahimiza Wakenya kuzingatia kinachounganisha NASA ambacho ni haki katika uchaguzi, asasi huru za umma ikiwa ni pamoja na mahakama, vyombo vya habari na kuimarisha ugatuzi.

“Niko NASA kwa sababu ninajua mizizi yake na ninaelewa malengo yake, mtu asifikirie kukosa kujumuika pamoja Uhuru Park kulibadilisha chochote,” alisema Bw Mudavadi.

Miongoni mwa waliohudhuria ni seneta wa kaunti ya Busia  Amos Wako, Mwakilishi wa wanawake kaunti ya Vihiga Beatrice Adagala, Wabunge Sakwa Bunyasi (Nambale), Tindi Mwale (Butere), Omboko Milemba (Emuhaya), Christopher Aseka (Khwisero), Ayub Savula (Lugari), Alfred Agoi (Sabatia) na Ernest Ogesi (Vihiga).