AU yalaani ghasia Eswatini maandamano yakichacha

AU yalaani ghasia Eswatini maandamano yakichacha

Na MASHIRIKA

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

MUUNGANO wa Afrika umelaani ghasia, uporaji na uharibifu wa mali unaoendelea Eswatini huku maandamano dhidi ya serikali yakichacha.

Mwenyekiti wa tume ya muungano huo, Moussa Faki Mahamat, amesema kwenye taarifa kwamba anafuatilia kwa karibu hali katika nchi hiyo na anasikitishwa na hali inayoendelea ya kisiasa na usalama.

“Mwenyekiti anahimiza hatua za haraka kuchukuliwa kulinda raia na mali yao, na anahimiza viongozi wa Eswatini na wadau kukomesha vitendo vya ghasia ambavyo vinaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi,” ilisema taarifa ya Bw Mahamat.

Alihimiza pande zote kujadiliana miongoni mwao kutatua mzozo uliopo huku akiahidi usaidizi wa AU kwa serikali na watu wa Eswatini.

Maandamano yalianza mwishoni mwa wiki jana watu wakimtaka Mfalme Mswati kujiuzulu na kupisha utawala wa demokrasia. Waandamanaji wanataka kuwe na kipindi cha mpito katika nchi hiyo kupisha utawala wa demokrasia.

Eswatini ambayo awali ilifahamika kama Swaziland ndiyo nchi ya pekee barani Afrika inayokumbatia kikamilifu utawala wa ufalme.

Maandamano yalianza kwa amani kabla ya ghasia kuanza na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku maduka yakivunjwa, nyumba na magari kuchomwa. Shamba la miwa pia lilichomwa na waandamanaji hao.

Waandamanaji waliokuwa na hasira walisemekana kulenga biashara zinazohusishwa na Mfalme Mswati 111 na mali ya serikali.

Maandamano hayo yalianzia eneo la Manzini Juni 20 wakati vijana walipoingia barabarani wakitaka haki ya kuchagua waziri mkuu kidemokrasia. Kwa wakati huu ni Mfalme Mswati anayeteua waziri mkuu.

Pia walimtaka Mfalme Mswati aruhusu demokrasia katika nchi hiyo.

Hali ilichacha Juni 28 majengo yalipochomwa na maduka kuporwa katika mji wa Matsapha.

Ghasia zilizidi baada ya Kaimu waziri mkuu Themba Masuku kupiga marufuku watu kuwasilisha malalamishi kwa kitengo cha utawala cha kitamaduni kinachoitwa Tinkhundla.

Kulingana na shirika la Swaziland Solidarity Network (SSN), raia wa eSwatini walikuwa na mfumo wa kulalamikia serikali kwa kuwasilisha malalamishi kwa Tinkhundla.

“Serikali imepewa muda hadi mwisho wa Julai kujibu matakwa yote katika malalamishi na ikikosa kufanya hivyo yatawasilishwa kwa wasimamizi wa majimbo,” alisema msemaji wa SSN Lucky Lukhele kwenye taarifa.

Alisema serikali ilikasirisha watu kwa kupiga marufuku mfumo huo wa kutoa malalamishi.

You can share this post!

Presha Gavana Joho aseme Shahbal tosha

Uhispania wazamisha Uswisi kupitia penalti na kufuzu kwa...