Habari Mseto

Aua bosi wake kupinga masharti makali ya kazi

February 6th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME mmoja kutoka kaunti ya Uasin Gishu ameshangaza wakazi, baada ya kumuua mwajiri wake akidai kuwa alikuwa na masharti makali.

Mwanaume huyo kwa jina Felix Kipkosgey Kibet wa miaka 30 alikuwa akifanya kazi za vibarua vya shambani nyumbani kwa Bi Jepkorir Limo wa miaka 54, kabla ya kumuangamiza.

Hata hivyo, alikuwa amefanya kazi nyumbani kwa mama huyo kwa siku tano tu, lakini akaripotiwa kuwa kila mara alikuwa akilalamika kuwa masharti ya mama huyo kazini yalikuwa makali sana.

Siku ya tukio, mshukiwa anasemekana kumvamia marehemu alipokuwa akipika chakula saa saba mchana, akampiga kwa nyundo kichwani hadi kufa, kisha akafungia maiti yake jikoni na kutoweka.

Kisa hiki kilitokea katika kijiji cha Kamoiywo, eneobunge la Soy na mshukiwa anadaiwa kutorokea eneo la Keiyo kaskazini.

Bado polisi wanamwindam huku wafanyakazi wenza wakidai kuwa alikuwa amelalamikia ukali wa msimamizi wake na kusema kuwa hangevumilia.

“Kwa mara kadha alikuwa amelalamika kuwa yeye ni mwanaume aliyetahiri na hangekubali mwanamke kumzomea ovyo ovyo,” akasema mkazi ambaye walifanya vibarua pamoja.

Marehemu alipatikana akiwa maiti saa chache baada ya tukio.